HABARI

 

Sunday, September 16, 2012

HOJA MTAMBUKA

0 Comments
Tambwe Hiza
WAANDISHI WAMEANDAMANA SAWA, JE  TUISHIE   HAPO?

 
Na Richard Tambwe Hiza
WIKI hii waandishi wa habari kutoka katika vyombo mbalimbali nchini waliandamana kulaani kuuawa kwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Chanel 10 huko Iringa, kifo cha mwandishi huyu kwa bahati mbaya na kwa mara nyingine tena kimewagawa wananchi katika makundi yanayotofautiana kifikra kuhusu chanzo na hatimaye kufariki kwake. 
 
Wapo wanaoona na kuamini polisi wametumia nguvu kubwa katika kukabiliana na tatizo lililokuwepo, wapo wanaoamini kwamba jeshi la polisi lilikuwa linatimiza wajibu wake na madhara haya makubwa yaliyotokea yanatokana na CHADEMA kuendeleza ghasia katika nchi na  kujaribu kuifanya isitawalike kama walivyoahidi baada ya kushindwa vibaya katika uchaguzi mkuu uliopita (walishinda viti 23 kati ya majimbo 239).
 
Hata hivyo, kabla ya kuingia katika tafakuri pana zaidi zinazotokana na msiba huu sina budi kutoa pole kwa familia ya Mwangosi, waandishi waliokuwa karibu naye katika kufanikisha majukumu yake ya uandishi wa habari, Kituo cha Channel 10 na Watanzania wote kwa ujumla, kwa kuondokewa na mwananchi mwenzetu katika mazingira ambayo wote hatukuyategemea.
 
Tumeshuhudia wakati taifa likiwa katika simanzi nzito kutokana na msiba huu, wapo wenzetu walioamua  kuutumia kama turufu ya kuleta chuki baina ya jeshi la polisi na waandishi na zaidi umma wa Watanzania ambao usalama wao na mali zao unategemea sana uwepo wa jeshi hilo. Kuna mambo mengi ambayo nimekuwa najiuliza na ningependa Watanzania wote tujiulize, hivi ghasia zilizosababisha msiba huu zilisababishwa na nini/nani?
 
Je kulikuwa na ulazima kwa CHADEMA kukaidi amri ya polisi ya kusubiri sensa ipite? Je, ukaidi wa CHADEMA siyo chanzo cha maafa yaliyotokea na yanayotokea mara kwa mara nchini? Je, ingekuwa sawa kwa jeshi la polisi kuwaachia CHADEMA kufanya shughuli ambayo walikwisha wazuia wasiifanye? Je, polisi ingewaachia kufanya jambo ambalo walikwishawazuia  wangekuwa wanatimiza sheria na wajibu wao? Na je,  uhalali wa uwepo wa jeshi hilo ungeendelea kuwepo?
 
Wananchi wote tunapaswa kuheshimu sheria na polisi wana jukumu la kutulazimisha kufuata sheria tunapozikiuka vikiwemo vyama vya siasa, najua sheria ya vyama vya siasa inavipa fursa vyama kufanya maandamano na mikutano baada ya kutoa taarifa polisi, lakini sheria hiyo hiyo inasema vitafanya hivyo endapo tu kama havitapata amri pingamizi kutoka polisi (sheria ya vyama vya siasa 1992 kifungu cha 11).
 
Tujiulize kulikuwa na ulazima gani kwa CHADEMA ambao mwaka mzima wamekuwa wakiruhusiwa kufanya mikutano na maandamano kulazimisha kufanya mkutano uliosababisha kifo baada ya kupata amri pingamizi? Kama waliona polisi hawakuwafanyia haki je ilikuwa vyema kuandaa  mapambano dhidi ya polisi? Jje walichukua hatua yoyote ya kisheria dhidi ya polisi au hawana imani na vyombo vya kisheria kama ambavyo Tundu Lissu anavyoziponda mahakama zetu bila kuheshimu kwamba zilimpa  ushindi yeye binafsi katika kesi yake ya uchaguzi aliyofunguliwa na mgombea wa CCM, na zile zilizokipa ushindi chama chake zilizowavua ubunge wana CCM  huko Sumbawanga na Igunga.
 
Naamini ili jeshi la polisi liweze kuendelea kulinda amani ndani ya nchi ni lazima tuliamini na lazima tujue kwamba lipo, likizuia jambo kwa mujibu wa sheria wote tuheshimu vinginevyo litakuwa halina sababu ya kuwepo. Si mara moja au mbili mamlaka za umma na vyombo vya sheria viliamua mambo muhimu katika maendeleo ya taifa, lakini yalipata upinzani hadi pale polisi ilipotumia nguvu kuhakikisha sheria inafuatwa na utekelezaji wake unatimia. 
 
Je, kumfukuza waziri katika hafla ya kulaani mauaji na kumkaribisha mwana-CHADEMA Dk. Lweitama kuhutubia na kuilaani serikali ni sawa? Je,  ni sawa kulilaumu jeshi zima la polisi kwa tatizo lililojitokeza sehemu moja ya nchi tena katika kutimiza wajibu wao?  Kitendo cha kutowalaani walioanzisha uvunjaji wa sheria uliosababisha ndugu yetu Mwangosi kupoteza maisha katika umri mdogo kinaashiria nini kutoka katika taasisi zetu za habari? 
 
Hapa ndiyo maswali mengine yasiyo na majibu yanapoanza, kwa nini tamko lililotolewa na CHADEMA na lile la wanahabari yanashabihiana. Kwa nini wanahabari hawakuilaumu CHADEMA hata mara moja kwa kutokutii sheria na  kuanzisha ghasia zilizosababisha maafa ya ndugu yetu. Nadhani tunahitaji tafakuri pana zaidi. Je wametumwa? Wana hasira? au nao wameanza kushirikishwa katika  ajenda za siri dhidi ya serikali na vyombo vyake?
 
Wote tumesikitishwa na msiba huu sidhani kama ni vyema kuendelea kushambulia jeshi la polisi bali kuangalia nani ameanzisha sokomoko ili awajibishwe kisheria, kama ikibainika aliyeua ni raia wa kawaida sheria ichukue mkondo wake, pia ikibainika muuaji ni askari akiwa katika kutimiza majukumu yake ni vyema  taratibu za kijeshi  na mahakama zitumike badala ya kuendeleza chuki zisizo na msingi.
 
Tusijisahau wote tunawahitaji polisi kama ambavyo tulikuwa tunamhitaji ndugu yetu Mwangosi nikiwemo mimi niliyeshirikiana naye katika shughuli mbalimbali. Tusiwe na hasira maana wahenga walisema  hasira hasara. Tutafute suluhisho la yanayotokea yasijirudie.  
 

0 Comments:

Post a Comment