HABARI

 

Wednesday, October 10, 2012

KAMA CHADEMA INAAHIDI UONGO KWA MAREHEMU NANI ITAOGOPA KUNDANGAYA?

0 Comments

NA CHARLES CHARLES-PICHANI
MJANE wa mmoja kati ya wafuasi watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliouawa wakati wa maandamano ya vurugu, ghasia na kinyume cha sheria mjini Arusha hapo Januari 5, mwaka jana, Asia Omar, amekishutumu chama hicho kwa ‘kutafuna’ fedha za rambirambi zilizochangwa kwa ajili marehemu mumewe, Ismail Omar.

Asia ambaye aliachiwa watoto wadogo wawili na mumewe, alifichua siri hiyo alipokuwa akiongea kwenye mkutano wa chama cha Civic United Front (CUF), uliofanyika hivi karibuni katika Uwanja wa Levolosi mjini humo na kusema hadi sasa, viongozi wa Chadema bado hawajamkabidhi fedha hizo ambazo walichangisha kwenye Uwanja wa NMC Januari 6, mwaka jana, wakati wa kuaga mwili wa marehemu mumewe.

“Nimekuja hapa leo kuelezea machungu yangu. Nasikitika kwamba Chadema mbali na kuchangisha fedha za rambirambi za marehemu mume wangu, hadi leo sijaiona hata senti tano”, alisema huku akiangua kilio hadharani.

Alizitaja fedha alizopata tangu wakati huo hadi sasa kuwa shilingi milioni tano zilizotolewa na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mustafa Sabodo, lakini Chadema iliyotangaza kuiangalia familia yake baada ya mumewe kuuawa kwenye maandamano yake imemsusa na kumdhulumu haki yake.

Kutokana na kilio hicho, viongozi wa CUF mkutanoni walifanya harambee iliyokusanya kiasi cha shilingi 500,000 taslimu na kumkabidhi papo hapo.

Siku chache baadaye, Itika Mwangosi ambaye ni mjane wa aliyekuwa mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten katika mkoa wa Iringa, Daud Mwangosi naye aliibuka na kuwaomba waandishi wa habari wamsaidie kufuatilia rambirambi ya marehemu mumewe aliyoahidiwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa.

Alisema kuwa tokea padri huyo wa zamani atangaze kumlipia ada mtoto wa kwanza wa marehemu Mwangosi anayeitwa Nehemiah, yule ambaye jana, Jumatatu ameanza kufanya mitihani ya mwisho ya kuhitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Malangali iliyopo wilayani Mufindi, Iringa – palepale aliposoma baba yake mzazi – hakuna chochote alichopewa.

Akizungumza wakati wa maziko ya marehemu Mwangosi yaliyofanyika Septemba 3 huko Rungwe katika mkoa wa Mbeya, Dk. Slaa aliyeanza jaribio la kutaka kuuteka msiba huo tokea Iringa, alisema amezungumza na mdau wake ambaye aliahidi kubeba jukumu zima la kumsomesha Nehemiah kuanzia sasa hadi pale atakapoishia kielimu.

Lakini tokea kipindi hicho, Itika amesema hakuna mawasiliano yoyote yaliyofanywa kwake na Dk. Slaa, lakini akasema kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Asiye na Wizara Maalum) na Mbunge wa Rungwe Mashariki (CCM), Profesa Mark Mwandosya ambaye pia aliahidi kusimamia elimu ya kila mtoto wa familia hiyo sawa na kama baba yao mzazi angekuwa hai ndiye anayepatikana.

Mwandosya ambaye aliiwakilisha serikali katika maziko hayo, alisema atafanya hivyo kwa sababu marehemu alikuwa ni ndugu na jirani yake huko Rungwe, hivyo watoto aliowaacha ni sehemu ya familia yake.
“Nina mawasiliano na Profesa Mark Mwandosya”, anasema mjane huyo wa marehemu na kuongeza: “Yeye ameniambia nitakapokuwa tayari nimjulishe ili atume fedha kwenye akaunti ya shule, lakini sina mawasiliano na Dk. Slaa”.

Hiyo ndiyo sura “ya ndani” aliyonayo Dk. Slaa na viongozi wenzake wa Chadema. Kama ilivyoandikwa na gazeti moja litolewalo kila siku nchini, Ijumaa iliyopita, utamaduni mpya wa siasa za misibani unaoendana na mauaji yanayotokana na ukaidi wa wanasiasa kwa Jeshi la Polisi, hatimaye umeanza kukiumbua chama hicho kwa “kushindwa kutekeleza ahadi ndogondogo tu za kutoa rambirambi kinazowaahidi wafiwa”. 

Kimekuwa na ujasiri wa kutotii Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuvunja kwa makusudi sheria na kuendesha siasa za vurugu, ghasia na kila aina ya ubabe unaosababisha kuzuka kwa mauaji ya raia wasiohusika na chochote ambao hadi sasa idadi yao imefikia sita.

Watatu walipoteza maisha yao kwenye maandamano haramu mjini Arusha, Januari 5, mwaka jana, mmoja akauawa na vijana wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa chama hicho kilipofanya mkutano wa hadhara wilayani Iramba, Singida, Julai 14, mwaka huu. 

Mwingine aliyeingia katika orodha hiyo, Ali Zona, aliuawa katika maandamano mengine yaliyofanywa kinyume cha sheria eneo la Msamvu mjini Morogoro mwishoni mwa mwezi Agosti, mwaka huu pia.

Idadi hiyo inakamilishwa na Daud Mwangosi aliyeuawa katika kijiji cha Nyololo, wilaya ya Mufindi, Iringa, Septemba 2. Mauaji hayo yalitokea wakati askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Jeshi la Polisi Tanzania (PT), wakijaribu kuuvunja mkutano wa hadhara wa Chadema uliokuwa ukifanyika kinyume cha sheria.

Katika kipindi hicho, mikutano yote ya kisiasa nchini isipokuwa ya kampeni za uchaguzi mdogo wa kiti cha uwakilisha katika jimbo la Bububu huko Zanzibar, ilikuwa imepigwa marufuku ili kupisha sensa ya watu na makazi.

Mara nyingi nimekuwa nikionyesha kiasi gani viongozi wa Chadema walivyo waongo na kuwaonya Watanzania, kwamba waepuke kuamini ghiliba na siasa zenye malengo haramu kwa taifa lao.

Viongozi wa Chadema kutoka wa kitaifa, mikoa, wilaya, majimbo, kata hadi vijiji na mitaa wamekuwa wakijifanya wasamaria na watu waliojazwa roho mtakatifu, hivyo mara zote yanapofanyika mauaji yanayosababishwa na chama hicho chenyewe wanatoa kauli pamoja na ahadi za kuvutia ili kuwadanganya Watanzania.

Kila mahali wanapofanya vurugu na ghasia zinazosababisha umwagaji wa damu hujitokeza hadharani na kuishutumu serikali kwamba “inaua watu ili kuilinda CCM”, kisha wanaahidi kufanya kila wanavyoweza kuzisaidia familia za marehemu ili “kuzifuta machozi”.

Wanaahidi kuzisaidia kifedha, kuzisomeshea watoto hasa walioachwa na baba zao wazazi au walezi wao, lakini kwa kawaida hufanya hivyo wakilenga kupata wanachama na wafuasi wa chama chao. Ndiyo maana wanafanya hivyo hadharani badala ya kuongea faragha na wafiwa ili kujua undani halisi wa matatizo yatakayowakabili.

Kama inavyosema Biblia Takatifu ambayo Dk. Slaa mwenyewe aliyewahi kuwa Padri wa Kanisa Katoliki anaifahamu vyema hata kama alishindwa kuitumikia, mtu anapotoa msaada hapaswi kufanya hivyo hadharani isipokuwa iwe kwa siri baina yake na aliyemsaidia katika hali yoyote.

Kinasema kitabu hicho kwamba kinachotolewa na mkono wa kulia “hata mkono wa kushoto usijue”, hivyo inashangaza kuona kasisi huyo wa zamani anashindwa kukiheshimu wakati alipaswa aonyeshe mfano kwa wenzake.

Badala ya kuheshimu maandiko hayo matakatifu, Dk. Slaa amekuwa kinara wa kupenda kujionyesha ili kutafuta sifa na kuzidi kuwaghilibu akili Watanzania, halafu kibaya zaidi ni pale anaposhindwa kutekeleza ahadi zote anazotoa na kuwa muongo aliyepitiliza.

Najiuliza mengi kuhusiana na suala hilo, moja kati yake ni kama chama hicho kinavunja sheria kwa makusudi kwa kuitisha mikutano kinyume cha sheria, kisha inapozuiliwa na vyombo vinavyohusika hufanya vurugu na kulilazimisha Jeshi la Polisi kuingilia kati.

Katika kufanya hivyo, yapo maeneo ambako hutokea bahati mbaya kuwa baadhi ya watu wasio na hatia yoyote hupoteza maisha yao kama wale waliouawa Arusha, mwaka jana.

Wanakuwa hawana hatia kwa sababu wanapandikiziwa uzushi, uongo, hasira, fitina pamoja na kila aina ya ukatili na kuwa wendawazimu vichwani. Wakifikia hali hiyo ndipo hujitolea mhanga kupambana na polisi, kuwapiga watu wasiotaka kuungana nao katika maandamano yao, kupora mali zao, kuchoma moto magari na majengo mbalimbali yakiwemo ya biashara mbali na kufanya uharibifu mwingine mkubwa.

Waliokuwa Arusha, mwaka jana, watakumbuka jinsi waandamanaji waliolishwa sumu ya chuki na hasira walivyokuwa ‘wamechanganyikiwa’ akilini, wakapita barabarani huku wakirusha mawe kwa watu wasiotaka kuandamana, wakayachoma moto baadhi ya maduka na kutaka kuliteketeza kwa namna hiyo pia jengo la makao makuu ya CCM la mkoa huo. 

Wakiwa katika hali hiyo ya uendawazimu uliopitiliza, waandamanaji hao waliochochewa na viongozi kama Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na Dk. Slaa walijaribu pia kufanya uhalifu mwingine mkubwa kupindukia.

Walikwenda huku wakiimba nyimbo za “pepole’s power” na kujaribu kuteka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, jaribio ambalo kama wangelifanikisha, jambo kubwa la kwanza lingekuwa ni kuvamia ghala la silaha na kuziiba zote, kisha wangewaachilia huru watuhumiwa mbalimbali wa uhalifu ukiwemo wizi wa kawaida, ujambazi wa kutumia nguvu na kadhalika na kuhitimisha kazi hiyo kwa kuliteketeza kwa moto jengo hilo lisiwepo tena.

Hapo jiji la Arusha na vitongoji vyake lingegeuka kuwa uwanja wa uporaji, ujambazi na mauaji yakiwemo ya kikatili na kila aina ya uhalifu. Ndiyo maana ilibidi polisi wawadhibiti kwa kuwarushia risasi za moto baada ya kutotishika na zile zilipopigwa kuelekea hewani ili watawanyike.

Ilikuwa wakati huo ndipo watatu kati yao akiwemo Ismail Omar walipopoteza maisha yao huku wengine kadhaa wakijeruhiwa, hatua iliyotoa mwanya kwa Chadema kuwachangisha fedha wananchi kwenye Viwanja vya NMC, kesho yake na kuwadanganya wafiwa akiwemo Asia kuwa wangepewa kama rambirambi lakini hadi leo, mwaka mzima na miezi tisa baadaye bado hawajapata hata senti tano!

Bahati mbaya kijana aliyeuawa katika kijiji cha Ndago, wilaya ya Iramba mkoani Singida alikuwa ni kiongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), hivyo isingewezekana kwenda kuwadanganya wazazi wake kwa namna yoyote. Ilikuwa vigumu kwa sababu walijua kuwa ndugu zake hawawezi ‘kudanganyiwa pipi’ na kujiunga Chadema.

Lakini alipouawa mtu mwingine kule Morogoro, viongozi wa Chadema walijaribu kuuteka msiba wake ili uwe wao, wakataka wauchukue na kuusimamia kwa kila kitu na hatua zake zote kuanzia hospitali ulikopelekwa mwili wake hadi nyumbani kwao huko Tanga, juhudi ambazo hata hivyo ziligonga mwamba.

Ndiyo maana haikuwa ajabu siku chache baadaye kumuona Dk. Slaa akiongoza vurugu nyingine kubwa huko Iringa, zile ambazo hatimaye zilisababisha kifo cha Mwangosi.

Akataka pia kuuteka msiba ule ili uwe wa Chadema na siyo wa familia ya marehemu kutoka nyumbani kwake, Kihesa Kilolo katika mji wa Iringa hadi kwenye maziko yake huko Rungwe, mkoa wa Mbeya, lakini juhudi hizo nazo zikadhibitiwa na Klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Iringa (IPC) katika sehemu hizo zote.

Hapo ndipo akamwahidi mjane wa marehemu, Itika kuwa angemsomeshea mtoto wake, Nehemiah anayesoma Shule ya Sekondari ya Malangali, lakini kama alivyomdanganya Asia Omar kule Arusha, yeye pia ameshindwa kumpa chochote kwa sababu alikuwa akitaka sifa na siyo vinginevyo.

Alikuwa akitaka umaarufu wa kisiasa kwake binafsi kama Dk. Slaa. Alikuwa akikihangaikia chama chake ili kipate wanachahama zaidi. Alikuwa akiendeleza mfumo wake wa kutumia misiba kusaka mamlaka mwaka 2015 maana ameahidi kuwa Chadema ni lazima ishinde na kutinga Ikulu, hivyo anahofia kwamba ikishindwa naye atakuwa moja kwa moja amekwisha kisiasa.

Lakini swali kubwa la kujiuliza hapa ni je, kama chama hicho kinaahidi uongo hadi kwa marehemu waliokufa katika vurugu zake chenyewe kuwa kitawapa rambirambi wake zao, kuwasomeshea watoto wao na kisha ‘kinaingia mitini’, nani aliye hai ambaye kitaogopa kumdanganya ili kitawale?

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu Na. 0569 220 220 na 0762 633 244

0 Comments:

Post a Comment