Marehemu Daud Mwangosi |
DAR ES SALAAM, TANZANIA
SERIKALI imetoa taarifa ya uchunguzi wake kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwandishi wa Channel Ten Daudi Mwangosi, kilichotokea mkoani Iringa mwezi uliopita.
Tariifa hiyo pamoja na mambo mengine imeainisha kwamba, hatua ya viongozi wa Chadema kukataa kutii amri halali ya Polisi ndio chanzo cha vurugu zilizosababisha kifo cha mwandishi huyo.
Pia taarifa hiyo imesema tukio la kuuawa kwa Mwangosi, Septemba 2 mwaka huu, lilitokea baada ya Operesheni ya Polisi mkoani hapo kumalizika, hasa baada ya CHADEMA kung’ang’ana kukusanyika isivyo halali eneo la Nyololo, mkoani hapo pamoja na kuzingatia uwepo wa ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa.
Dk. Slaa alimwandikia ujumbe mfupi wa maneno Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema uliokuwa ukisema “IGP nasubiri simu yako. Wajulishe Polisi wako waandae risasi zakutosha, mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji na kisha kusherehekea, mjiandae kwa kwenda mahakama ya Den Hague. Ni afadhali tufe kuliko manyanyaso haya”.
Kitendo cha ujumbe huo wa Dk.Slaa ni ishara tosha uliashiria umwagaji wa damu na ni ushaidi tosha kuwepo kwa uvunjifu wa amani kwa kuwa CHADEMA ndiyo chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani katika kijijini hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji Mstaafu, Steven Ihema alisema taarifa hiyo imetokana na Kamati kufanya mahojiano na watu mbalimbali waliokuwepo kwenye tukio hilo ikiwemo kupitia nyaraka na vielelezo mbalimbali, kutembelea eneo la tukio na ushahidi kutoka kwa waandishi wa habari.
Alisema kamati hiyo ilipewa hadidu za rejea sita ambazo ni uhalali wa mkusanyiko ulioitishwa na CHADEMA eneo la Nyololo na kuwepo kwa uvunjifu
wa amani, kama yalikuwepo makubaliano au maelekezo kuhusu mikutano ya hadhara au maandamano nchini katika kipindi cha Sensa, mazingira yaliyosababisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu iliyosababisha kifo na wengine kuumizwa.
Hadibu nyingine za rejea walizopewa ni uwiano wa nguvu hiyo na tukio, madai ya kuwepo uhasama kati ya Jeshi la Polisi na waandishi wa habari
mkoani humo na chanzo cha uhasama huo. Aidha kuna madai ya kuwepo kwa orodha ya waandishi watatu ambao Jeshi la Polisi limepanga kuwashughulikia.
Alisema zingine ilikuwa ni uwepo wa sheria, kanuni au taratibu zinazotoa uwezo kwa Jeshi la Polisi kuzuia mikusanyiko inayoitishwa na vyama vya siasa na mamlaka ya rufaa endapo vyama hivyo havitaridhika na amri hizo na hali ya mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na vyama vya siasa nchini katika utendaji kazi wao na utii wa sheria.
Jaji Ihema, alisema kamati ilifanya mahojiano na watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na watendaji wa serikali hususan, kamati za ulinzi na usalama ngazi ya wilaya Mufindi na mkoa wa Iringa viongozi wa Jeshi la Polisi viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa madhehebu ya dini, waandishi wa habari na wananchi wa kawaida ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa na taifa.
Alisema matokeo ya uchunguzi kutokana na hadibu za rejea yanaonyesha kuwa kuwepo kwa zuio la mikutano ya siasa ya CHADEMA mkoani Iringa wakati wa
Sensa ya Watu na Makazi linathibitishwa na amri ya utendaji ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda pamoja na barua ya msajili wa vyama vya siasa.
Jaji huyo alisema pamoja na zuio la mkutano huo viongozi wa CHADEMA walikataa kutii amri hiyo na kwamba kutokana na taarifa hizo kamati ya uchunguzi inathibitisha kwamba hapakuwepo na uhalali wa mkusanyiko au mkutano ulioitishwa na CHADEMA eneo la Nyololo, Wilaya ya Mufindi.
Alisema kwa mujibu wa maelezo ya kamanda wa polisi mkoa wa Iringa, mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia cha mkoa huo na Joseph Senga ambaye ni mpiga picha na mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima tukio la kuuawa kwa Mwangosi lilitokea baada ya Operesheni ya Jeshi la Polisi kumalizika.
Jaji Ihema alisema kitendo cha kutotii amri halali ya Kamanda wa Polisi kuagiza wafuasi wa CHADEMA watawanyike kutoka kwenye eneo la ofisi ya kata ya CHADEMA ilikuwa chanzo cha vurugu hizo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, kamati ya uchunguzi imethibitisha kwamba maelekezo kwa vyama vya siasa kutoendesha shughuli za mikutano ya hadhara au maandamano yalitolewa kwa mujibu wa sheria katika kipindi cha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.
Alisema hapakuwa na uwiano wa bomu na tukio la mauaji kwa vile utaratibu wa matumizi ya bomu hilo unaelekeza kulenga juu usawa wa nyuzi 45
na umbali mita 80 mpaka mita 100.
Jaji huyo alisema hapakuwa na uhalali wa kutumia bomu la kishindo kwani lengo la ulipuaji wake ni ili watu waogope na kukimbia na kwamba kamati imeona nguvu iliyotumika mwanzo hadi kumaliza Operesheni haikuwa kubwa na kuongeza kuwa tukio la kuuawa kwa Mwangosi na kuumizwa baadhi ya askari polisi halikustahili.
Akizungumzia mgogoro uliopo baina ya polisi na waandishi wa habari mkoani Iringa, alisema kamati inapendekeza taasisi za habari zinazosimamia maadili na weledi wa vyombo vya habari, hususan Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jukwaa la Wahariri wafanye utaratibu unaostahiki za upatanishi kati ya waandishi wa habari, Jeshi la Polisi na uongozi wa mkoa wa Iringa na hali hiyo itasaidia kurejesha uhusiano mzuri kati ya vyombo hivyo muhimu katika mkoa.
Alisema changamoto zilizojitokeza katika uchunguzi ni pamoja na Jeshi la Polisi kukosa mafunzo endelevu, ukosefu wa majukumu katika utekelezaji wa majukumu yake, vyama vya siasa kukosa uvumilivu katika kuendesha shughuli zao na uelewa mdogo wa baadhi ya viongozi wa vyama kuhusu uendeshaji wa
vyama vya siasa.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema kamati hiyo ilifanya kazi kubwa na Watanzania wote wananafasi sawa.
Wakati huo huo, Baraza la Habari Tanzania(MCT) imetoa taarifa yake kuhusiana na mauaji hayo, baada ya tume waliyounda kushirikiana na Jukwaa la Wahariri kumaliza kazi yake.
Katibu Mtendaji wa MCT Kajubi Mukajanga alisema tume hiyo imemaliza kazi yake na kuonyesha kuwa Mwangosi aliuawawa na askari kwa maagizo ya Kamanda Kamuhanda.
"Kwa maksudi kabisa Polisi waliwashughulikia waandishi wa habari wa Iringa wakati wakikusanya taarifa kuhusiana na CHADEMA eneo hilo,''alisema.
Hivyo, alisema taarifa hiyo itapelekwa bodi pamoja na kufanya vikao vya pamoja kati ya MCT na Jukwaa ili kutolewe kwa tamko la pamoja kuhusiana na taarifa hiyo.
0 Comments:
Post a Comment