Kwa taaluma, Naibu Waziri Nkamia (Pichani) ni mwanahabari ambaye
amesomea na kufanya kazi ya habari kwa kipindi kirefu kabla ya kuingia katika
Ubunge ambao umemuwezesha kuteuliwa kuwa waziri.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili
katika wizara hiyo, Nkamia alisema anamshukuru Rais Kikwete kwa kumteua na kumpa dhamana
hiyo na kuahidi kuwa atasaidiana na Waziri wa wizara hiyo kutimiza majuku ya
wizara katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya nne.
“Kama kiongozi mwenye mamlaka ndani ya wizara hii, nipo
tayari kushirikiana na viongozi wenzangu katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo kupitia Idara zote zinazounda wizara hiyo”, alisema.
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inaundwa na
idara kuu nne za kisekta ambazo ni Idara ya Habari, Idara ya Vijana, Idara ya
Maendeleo ya Utamaduni na Idara ya
Maendeleo ya Michezo.
Kwa kuwa tasnia ya habari ni miongoni mwa idara zilizo chini
ya wizara hii, Nkamia alisema kuwa yupo tayari kushirikiana na wadau wa habari
ikiwemo kusimamia maslahi ya waandishi wa habari nchini.
“Ukitaka kujua umuhimu wa vyombo vya habari na waandishi wa
habari katika nchi yeyote ile, jaribu kuvifanya
vyombo hivyo kuanzia redio, televisheni na magazeti visifanye kazi hata
kwa muda wa saa moja tu uone ni hasara kiasi gani na hatari kiasi gani
zitatokea katika nchi ile” alisema Nkamia.
Alisema anaheshimu na
anatambua umuhimu wa vyombo vya habari na waandishi wa habari nchini na
atafanya nao kazi vizuri kwa kipindi chote atakachokuwa wizarani hapo.
Alisema kuwa anatambua kuwa waandishi wa habari wanafanya kazi katika mazingira magumu wakati wa
kutekeleza majukumu yao ikiwemo tatizo
la “ukanjanja” na lugha mbalimbali zinozotolewa juu yao.
Amaeahidi kushirishirikiana na viongozi na wadau wa habari
kuhakikisha kinaundwa chombo (bodi) kitakachosimamia maslahi ya waandishi wa
habari.
Bodi itakayoundwa itasaidia kusimamia tasnia ya habari na
kuhakikisha habari zinazoandikwa zitakuwa kwa maendeleo, manufaa na maslahi ya
taifa na kuhakikisha inawajengea heshima waandishi wenyewe kwa kazi zao
wanazofanya kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao na ya nchi.
Naibu Waziri Nkamia ametoa rai kwa wadau wote wa habari
kushirikiana ili kufanikisha uundwaji wa sheria ya habari. Alisema “Sheria hii
ikikamilika itasaidia kuboresha baadhi ya changamoto za wanahabari ikiwemo
ajira zao na mafao yao ya sasa na uzeeni”.
Nkamia amepewa wadhifa
huo baada ya Rais Dkt. Kikwete kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri
katika kuziba nafasi zilizoachwa na mawaziri wanne waliojiuzulu na mmoja
aliyefariki mwanzoni mwa mwezi huu.
Nkamia
ni mkongwe aliyebobea katika taaluma ya uandishi wa habari akiwa amefanya kazi
na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi.
Aliajiriwa
kwa mara ya kwanza na Redio ya Taifa (Radio
Tanzania Dar es Salaam) mnamo Oktoba 10, 1994 kama mwandishi msaidizi. Alifanya
kazi RTD kwa muda wa miaka tisa hadi 2003 alipojiunga na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika
la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Akiwa
BBC Nkamia alifanya mambo mengi mazuri yaliyomjengea heshima mwenyewe na taifa.
Ikizingatiwa kuwa Nkamia alipenda sana kutangaza
habari za michezo, alifanikiwa kutangaza mechi mbalimbali za ndani na nje ya
nchi.
Kama
mwandishi wa habari za michezo, Nkamia alikuwa Mwafrika na Mtanzania wa kwanza
kutangaza mchezo wa mpira wa miguu wa ligi ya Uingereza kwa lugha ya Kiswahili.
Kutokana
na umahiri wake katika kutangaza habari za michezo, Nkamia aliaminiwa kutangaza
mchezo wa fainali ya ligi ya Uingereza mwaka 2006 kati ya Manchester United na
Arsenal na mwaka huo huo, BBC ilimpa
tena jukumu la kutangaza mechi ya fainali ya Ligi ya klabu bingwa ya Ulaya kati
ya Arsenal na Barcelona.
Mwaka
2006 Nkamia alirudi nyumbani Tanzania na kujiunga na Shirika la Utangazaji la
Taifa (TBC) ambapo alifanyakazi kama mwandishi na mhariri hadi 2009.
Mwaka
2009 hadi 2010 Nkamia alifanya kazi ya uandishi katika shirika la utangazaji la
Sauti ya Amerika (VOA) inayomilikiwa na Taasisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya
Marekani kazi ambayo aliifanya kwa mwaka mmoja.
Mwaka
2010 Nkamia alitambua na kuitikia dhamiri yake ya kuitumikia nchi yake katika
mambo ya siasa hivyo aliamua kurudi Tanzania kuomba ridhaa ya wana Kondoa Kusini
awe mwakilishi wao bungeni na Kamati Kuu ya chama chake, Chama cha Mapinduzi, ikapitisha
jina lake kuwa mgombea ubunge wa chama hicho jimboni humo.
Nkamia
anasema, kwa kuwa alikuwa anafanya kazi na watu, wapo waliomshagaa kuacha kazi
ya maslahi zaidi na kurudi nyumbani. Miongoni mwa hao ni Dkt. Shaka Ssali mtangazaji
na mmoja wa wanahabari maarufu duniani
aliyeuliza Nkamia anafanya nini katika
karne yenye changamoto ya ajira duniani kuacha kazi yenye mshahara na maslahi
makubwa na kwenda kwenye siasa.
Anasema
kwake jibu la swali hilo lilikuwa rahisi kuwa ni Uzalendo wa nchi kwanza ndiyo
maana aliamua kurudi kutoa mchango wake
kwa maendeleo ya watu wake wa Kondoa Kusini na nchi kwa ujumla.
Kwa
kuzingatia ukomavu na weledi alionao kwenye taaluma ya habari, ndiyo maana Mhe.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete ameamini na kumpa
dhamana ili asaidiane na Waziri mwenye
dhamana katika Wizara hiyo, Fenella Mukangara, kuiongoza Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo.
Nkamia
amechukua nafasi hiyo badala ya Mhe. Amosi Makalla aliyehamishiwa Wizara ya
Maji.
Wengine
waliowahi kushika nafasi ya Naibu Waziri katika wizara hiyo ni Dkt. Makongoro
Mahanga, N. Nswanzungwanko, Joel Bendera, Dkt. Emmanuel Nchimbi na Dkt.Fenella
Mukangara ambaye sasa ni waziri wa wizara hiyo.
Juma Nkamia ni mtoto wa tatu kuzaliwa kati ya watoto sita
wa familia ya Mzee Selemani Nkamia na Mwanaidi Ndwata. Anatokea eneo la kanda
ya Kati katika mkoa wa Dodoma wilayani Kondoa. Ni baba wa familia mwenye mke mmoja Bi Amina
na watoto wawili ambao ni Kassi mwenye umri wa miaka 13 anayesoma kidato cha
pili Shule ya Sekondari ya Wavulana Fezza na Hassani mwenye umri wa miaka
saba anayesoma darasa la pili katika shule hiyo hiyo.
Kwa sasa Nkamia anaendelea kujiimarisha kielimu akiwa anasoma
katika chuo Kikuu cha Dodoma. Makala hii tumeitoa bila kuongeza au kupunguza chochote kama ilivyoandikwa na Eleuteri Mangi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Mtayarihaji Mkuu, theNkoromo Blog
0 Comments:
Post a Comment