Hivi Punde!

BURUNDI YAMTUNUKIA TUZO MWALIMU NYERERE

Akabidjiwa Rais Kikwete tuzo hiyo mjini Bujumbura
Mwalimu Nyerere
BUJUMBURA, BURUNDI
Taifa la Burundi limemtunukia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere Tuzo la juu kabisa ambalo Burundi hutoa kwa watu mbali mbali kutokana na mchango wake katika kuleta uhuru na baadaye kwa jitihada zake kubwa za kuleta amani katika nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imesema Mwalimu Nyerere alitunukiwa Tuzo hiyo ya Order of the National Republic of Burundi, kwenye Kilele cha Sherehe za Kuadhimisha Miaka 50 ya Uhuru wa Burundi zilifanyika jana, Independence Road, pembeni mwa Uwanja wa Michezo wa Louis Rwagasore mjini Bujumbura na kutangazwa hadharani kwa maelfu kwa maelfu ya watu waliohudhuria sherehe hizo.
"Tuzo hiyo ya Mwalimu imepokelewa kwa niaba yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alikuwa mmoja wa viongozi sita wa nchi za nje waliohudhuria sherehe hizo", imesema taarifa hiyo.
Akitangaza Tuzo hilo, Rais wa Burundi, Mheshimiwa Pierre Nkurunzinza alisema kuwa Burundi imeamua kumtunuku Mwalimu Nyerere kutokana na sababu mbili; moja ni ushauri wake muhimu sana katika kuleta uhuru wa Burundi kutoka kwa wakoloni wa Kibelgiji.
“Kwanza Mwalimu alikuwa mshauri muhimu sana wa Mwanzilishi wa Taifa letu, Mheshimiwa Louis Rwagasore na baadaye zilikuwa ni jitihada zake ambazo hatimaye zimeleta amani na utulivu ambao tunaufurahia katika Burundi kwa sasa,” imenukuu taarifa hiyo
Pamoja na Hayati Mwalimu, aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela pia amepata tuzo hiyo. Mzee Mandela alichukua nafasi ya Mwalimu kama mpatanishi wa mgogoro wa Burundi kufuatia kifo cha Mwalimu mwaka 1999.
Katika sherehe hizo, zilizoendelea mfululizo kwa saa saba unusu tokea saa nne asubuhi hadi saa 11 jioni, Rais Kikwete aliungana na viongozi wenzake wa nchi sita na wawakilishi wa nchi nyingine nyingi duniani kuhudhuria kilele cha sherehe za kufana kuadhimisha Miaka 50 ya Uhuru wa Burundi.
Burundi ilipata uhuru kutoka kwa wakoloni wa Kibelgiji Julai 2, mwaka 1962 na Rais Kikwete aliwasili Bujumbura asubuhi ya jana, akitokea Kigali, Rwanda, ambako pia alihudhuria sherehe kama hizo Kuadhimisha Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Rwanda iliyopata uhuru Julai Mosi, 1962, kutoka kwa wakoloni hao hao wa Kibelgiji.
Tofauti na Rwanda ambako Rais Kikwete alikuwa rais pekee aliyehudhuria sherehe za uhuru wa nchi hiyo na mgeni rasmi, katika sherehe za Burundi, Mheshimiwa Rais na Mama Salma Kikwete wameungana na Rais mwenyeji Pierre Nkurunzinza, Rais Mwai Kibaki wa Kenya, Rais Theodore Obing Nguema wa Equatorial Guinea, Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Rais Shariff Sheikh Ahmed Shariff katika kusherehekea uhuru wa Burundi. 
Walikuwepo wawakilishi wa nchi nyingine nyingi duniani akiwamo Makamu wa Rais wa Uganda na Makamu wa Rais wa Nigeria, Mheshimiwa Prince Philip ambaye ni mtoto wa Malkia wa Belgium, Waziri Mkuu wa Swaziland na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) anayemaliza muda wake, Mheshimiwa Jean Ping.
Wananchi wa Burundi wamejitokeza kwa wingi sana kuhudhuria sherehe za uhuru wa nchi yao ambayo tokea mwaka 1965 yalipotokea mapinduzi ya kijeshi ya kwanza haijapata kuwa na raha ya kuwa na amani kwa miaka 10 mfululizo ukiondoa sasa.
Moja ya mambo ambayo yamechukuwa muda mrefu kiasi cha saa tatu ni maandamano ya wananchi wa Burundi ambayo yameshirikisha vikundi vya wananchi kutoka taasisi mbali mbali zikiwamo Idara za Serikali, Makampuni Binafsi na Taasisi Zisizokuwa za Kiserikali.
Askari wa miavuli wakiwa wamebeba bendera za Taifa la Burundi pia wamekuwa kivutio kikubwa katika sherehe hizo kama yalivyokuwa maonyesho ya makomando wa Jeshi la Anga la Burundi (BAF)  kutoka kwenye helikopta iliyosimama angani hadi chini kiasi cha urefu wa mita 150.
Aidha, ngoma aina ya Rukinzo ilivutia sana wananchi kama lilivyokuwa gwaride la nchi tano Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambako kila kundi la askari wakiongozwa na kundi la askari wa Burundi lakini kila kundi likiwa chini ya kamanda wake lilipita mbele ya viongozi na maelfu kwa maelfu ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo.
Mbali na ngoma za vikundi vya ngoma za asili na utamaduni wa Burundi zimevutia sana hisia za wananchi,  pia wananchi kwenye sherehe hizo wameshuhudia gwaride la kuvutia la Jeshi la Burundi likiwa na vikosi mbali mbali kikiwemo Kikosi cha Kulinda Amani katika nchi mbali mbali duniani. Aidha, gwaride hilo limeshirikisha Jeshi la Polisi ambalo lilionyesha vifaa vya huduma mbali mbali ambazo hutolewa na Jeshi hilo  kulinda usalama wa raia zikiwamo za usalama barabarani, huduma za zima moto na huduma za magari ya kubeba wagonjwa.
Jeshi la Burundi pia limetumia nafasi ya sherehe hizo kuonyesha vifaa vinavyotumiwa na vikosi vya Jeshi hilo ambavyo ni Jeshi la Ardhini, Jeshi la Maji na Jeshi la Anga ikiwa ni pamoja na helikopta mbili za kijeshi –helicopter Gun Ships.
Rais Nkurunziza, mwenyeji wa sherehe hizo, ambaye alianza kuhutubia Taifa la Burundi kiasi cha saa 10 mchana, alitumia muda wa kutosha kuisifia Tanzania na uongozi wake wa awamu mbali mbali kwa mchango wake mkubwa katika uhuru wa Burundi na baadaye katika mazungumzo ya kuleta amani katika Burundi.
Alimsifia Rais Kikwete kama Rais wa nchi rafiki na jirani na kama “kaka yangu” katika hotuba hiyo ambako alitangaza kumtunukia medali ya juu kabisa katika Taifa la Burundi Mwalimu Nyerere kwa mchango wake katika Uhuru wa Burundi na baadaye katika kuleta amani ya nchi hiyo.
Rais Kikwete anatarajiwa kuondoka mjini Bujumbura baadaye leo, Jumanne, Julai 3, 2012, kurejea nyumbani.

No comments