Na Mwandishi Maalum, NEW YORK
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amemteua Naibu Katibu Mkuu anayemaliza muda wake, Dkt, Asha-Rose Migiro kuwa mjumbe wake maalum katika masuala ya ukimwi na ugonjwa wa ukimwi Barani Afrika.
Ban Ki Moon ametangaza uteuzi huo wakati wa hafla maalum aliyoiandaa mahsusi kwaajili ya kumuaga Naibu Katibu Mkuu wake,ambaye anahitimisha utumishi wake wa miaka mitano na nusu katika nafasi ya Unaibu katibu Mkuu.
Hafla hiyo imefanyika siku ya alhamisi katika viunga vya Umoja wa Mataifa, na kuhudhuriwa na wageni waalikwa mbalimbali wakiwamo mabalozi na wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa.
“Ninatangaza rasmi kwamba ninamteua dkt. Asha- Rose Migiro kuwa mjumbe wangu maalum katika masuala ya ukimwi na ugonjwa wa Ukimwi Barani Afrika. Akasema Ban Ki Moon tangazo lililoshangiliwa kwa nguvu na wageni waalikwa.
Akiongea kwa hisia, Ban Ki Moon, ameeleza kwamba ingawa Migiro alikuwa naibu katibu mkuu wake, lakini amekuwa mwalimu wake, amejifunza mengi toka kwake na daima ataendelea kuenzi mchango wake mkubwa.
“ Kama ni kuvaa viatu vyake, naweza kusema ningechekesha sana, kwa ufupi siwezi kuvaa viatu vya Migiro, amekuwa msaada mkubwa sana kwangu, ameniwakilisha vema kila mahali nilipomtuma hata katika mazingira magumu na ya hatari, kote ameniwakilisha vema sana, kama mwalimu wangu, na kama profesa wangu anastahili alama ya juu sana” akasema Ban Ki Moon na kushangiliwa.
Akamuelezea Migiro kama kiongozi si tu mwadilifu, lakini mwanadiplomasia aliyebobea, aliyefanya kazi kubwa,ngumu na nzito kwa moyo mkunjufu, uhodari , umakini, na uadilifu wa hali ya juu sana.
“ Siyo rahisi kuelezea yale aliyoyafanya nyuma ya pazia, namna gani alivyochapa kazi kwa nguvu, yapo mengi makubwa ambayo Migiro ameyafanya na kuyakamilisha kwa uadilifu wa hali ya juu. Migiro ni mwanadiplomasia aliyebobea lakini ni mtu wa vitendo, vitendo ambavyo lazima utaona matunda yake” akabainisha Ban Ki Moon
Na kuongeza “ Migiro amefanya kazi na viongozi wagumu, kiwamo aliyekuwa Rais wa Libya Muammar Quadaff aliyethubutu hata kumrushia katiba ya Umoja wa Mataifa, amezikuna nyonyo za watu wengi wakiwamo watu wanyonge na wenye matatizo mbalimbali. Migoro unaondoka, lakini Umoja wa Mataifa hauta sahau mchango wako. Hapa ni nyumbani kwako, na nitaendelea kuomba msaada wako na ushirikiano wako, bado nitaendelea kukuhitaji” akasisitiza Ban Ki Moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akatumia fursa hiyo kuishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kumruhusu Migiro kwenda kuitumikia jumuia ya kimataifa.
“ Ninapenda kutoa shukrani zangu za pekee kwa jamhuri ya muungano wa Tanzania, kwa kumtoa Migiro katika utumishi wake wa Umma kuja kunisaidia , kwa serikali ya Tanzania na watanzania nasema asanteni sana” akasema Ban Ki Moon..
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu dkt. Asha-Rose Migiro amesema anaupokea kwa mikono miwili uteuzi wa kuwa mjumbe maalum wa Katibu Mkuu katika masuala ya Ukimwi.
Akasema masuala ya ukimwi na ugonjwa wa ukimwi, ni eneo ambalo limo ndani ya moyo wake na kwamba anashukuru kuona kwamba Katibu Mkuu anamuamini kwamba anaweza kumsaidia. Akaahidi kwam atalitekeleza jukumu hilo kwa heshima kubwa.
Akamshukuru Ban Ki Moon, kwa kumuamini kwamba anaweza kumsaidia kama naibu Katibu Mkuu, na akamshukuru pia kwa ushirikiano mkubwa na uhusiano mkubwa uliojengeka kati yake na Ban Ki Moon lakini pia kati yake na wasaidizi wake. Ushirikiano ambao anasema ulichagiza utendaji kazi kufanikisha dira na matarajio ya Katibu Mkuu.
“Katibu Mkuu amenipa heshima ya kihistoria, heshima ya kuwa msadizi wake, ni heshima kubwa kwangu na kwa yeyote atakayekuja kuandika historia yangu, kwa namna yoyote ile hawezi kukwepa kumtaja Ban Ki Moon, naomba nikushukuru sana kwa heshima hii kubwa uliyonipa” akasema Migiro.
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na familia ya Naibu Katibu Mkuu ikijumuisha mume wake, Profesa Cleophas Migiro, mdogo wa Naibu Katibu Mkuu, Bi. Amina Mtengeti na mtoto wa mwisho wa Migiro Chansa Jasmin.
Naibu Katibu Migiro anakuwa mwanamke wa pili kushika wadhifa huo na mwanamke mwafrika wa kwanza. Lakini pia ni naibu katibu mkuu ambaye amehudumu katika wadhifa huo kwa miaka mitano na nusu.
0 Comments:
Post a Comment