HABARI

 

Tuesday, July 30, 2013

WAZEE WA KIMILA WAMPONGEZA MBUNGE WA TARIME NYAMBARI NYANGWINE

0 Comments
NYAMBARI NYANGINE
TARIME, Tanzania
SAISA chafu zinazodaiwa kuanza kushika kasi katika majimbo ya Tarime na Rorya, zimewaibua wanasiasa wakongwe na wazee wa kimila, ambao wametoa maonyo makali.

Pia, wamewataka wananchi kuendelea kuwaunga mkono wabunge Nyambari Nyangwine (Tarime) na Lameck Airo (Rorya), ili waendeleze kasi ya kuleta maendeleo.

Wamesema majimbo hayo kwa sasa yamekuwa mfano wa kuigwa nchini kutokana na maendeleo makubwa yaliyopatikana tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma, ambapo wamesema kamwe wanachama wanaoendesha siasa za makundi wasipewe nafasi kuwakatisha tamaa.

Sekta za elimu, afya na miundombinu katika wilaya hizo zimekuwa zikikua kwa kasi na serikali imejikita zaidi katika kuhakikisha maendeleo makubwa yanapatikana.

Waliyasema hayo mjini hapa jana kwa nyakati tofauti wakati wakizungumzia mwenendo wa kisiasa hasa baada ya baadhi ya makada wa CCM kudaiwa kuanza vurugu kwa kufanya kampeni chafu zenye lengo la kuwakwamisha wabunge hao.

Sinda Nyangore, ambaye ni Mwenyekiti wa Kimila kutoka koo 13, alisema wabunge hao wamezifanya wilaya hizo kupiga hatua kubwa kimaendeleo na kwamba, hawana budi kuungwa mkono ili kufanya mazuri zaidi.

Alisema siasa chafu ambazo wameanza kufanyiwa na makada wenzao ni hatari na zinaweza kuwakatisha tamaa katika kuwaletea maendeleo wananchi wao.

“Tumeimarika sana katika maeneo kwa sasa, tunahitaji kwa pamoja kuwaunga mkono Nyangwine na Airo ili watimize wajibu wao kwetu. Kuna mabadiliko makubwa kimaendeleo ikilinganishwa na miaka ya nyuma, sasa tunahitaji kwenda mbele zaidi na si kurudi nyuma na njia pekee ni kuwaunga mkono,” alisema.

Aliongeza kuwa majimbo hayo yameongozwa na wabunge wengi, lakini maendeleo ya haraka yameonekana wakati huu ambao wabunge hao vijana wanaongoza.

Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa CCM Wilaya ya Tarime, Dennis Zakaria, alisema siasa za makundi hazipaswi kuachwa zikaendelea kwani zimekuwa na madhara makubwa kwa ustawi wa Chama.

Alisema huu ni wakati wa Nyangwine na Airo kuwahudumia wananchi baada ya kupewa ridhaa hivyo, makada wengine kuanza kufanya kampeni kusala ubunge mwaka 2015 ni kinyume na taratibu.

Aliongeza kuwa kama Chama ni lazima wachukue hatua za haraka ikiwa ni pamoja na kuwaonya wahusika ili kutoa fursa kwa wabunge wa sasa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ambapo mpaka sasa mafanikio makubwa yamepatikana.


“Kuanza kampeni kabla ya wakati si utaratibu wa CCM, tunaelekezwa kuwasaidia waliopo madarakani kutekeleza Ilani na muda wa uchaguzi utakapofika basi uwanja hufunguliwa na kila mmoja kucheza. Kampeni chafu wanazofanyiwa hazikubaliki kabisa,” alisema Zakaria.


Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Rorya, Samwel Kiboye na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Pemba, Sigirya Mwita, walionya kuwa kampeni hizo zina lengo la kuwagawa wana-CCM na madhara yake ni kurejesha majimbo kwa wapinzani.


Kiboye alisema wana-CCM wanapaswa kukataa kugawanywa kwa maslahi ya wachache wenye uchu wa madaraka ili kuendelea kujenga umoja na mshikamano.

0 Comments:

Post a Comment