HABARI

 

Wednesday, October 9, 2013

ZANU-PF: WAAFRIKA VIPUUZENI VYAMA VYA UPINZANI

0 Comments
*Chadai ni mawakala wa Nchi za Magharibi
*Chahoji, kama Mugabe ni Mzee sana, mbona Malikia Elizabeth ni mzee zaidi ya Zimbabwe?

Katibu Mkuu, ZANU-PF,Mutasa, akizungumza leo
BASHIR NKOROMO, DSM
WATANZANIA na Waafrika kwa jumla wametakiwa kutovitilia maanani vyama vya upinzani kwa madai kuwa ni vya kibinafsi na havina mwelekeo wa kuwasaidia wananchi.

Wametakiwa kuendelea kukiamini na kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kiendelee kuongoza Tanzania kwa kuwa ndicho chama chenye sera na mtazamo wa uhakika wa maendeleo.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Chama tawala cha Zambia, ZANU-PF, Didymus Mutasa, katika mkutano wa sita wa Makatibu Wakuu wa Vyama vilivyokuwa vya ukjombozi kusini mwa Afrika,
uliofanyika leo, katika hoteli ya Kunduchi Beach, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Mutasa alisema vyama vya upinzani havina hadhi ya kuaminika sana kwa wananchi kwa sababu si vyama makinikutokana na uanzishwaji wake kuwa ni wa ubabaishaji jambo ambalo linavikosesha misingi ya kuweza kuleta maendeleo.

“Afrika hakuna vyama vya upinzani, Watanzania wasikubali kabisa, kwa kuwa vyama hivyo havina mwelekeo hasa kutokana na kutokuwa na mizizi katika uanzishwaji wake tofauti na vyama utawala ambavyo pamoja na kuanzishwa kwa lengo la kuzikomboa nchi zao lakini pia viliweka misingi ya kuinua uchumi,’’alisema.

Alizilaum nchi za Magharibi, akisema ndizo zimeleta utitiri wa vyama vya upinzani kwa lengo la kutafuta mianya ya kuja kunyonya na kupora rasilimali zilizo ndani ya Afrika, na kusisitiza kuwa waafrika wasikubali kuvipa nafasi.

Kuhusu chama chake cha ZANU-PF kuendelea kutwaa madaraka ya uongozi nchini Zimbabwe kupitia chaguzi mbalimbali, ukiwemo ulimalizika hivi karibuni na Rais Robert Mugabe kushinda Katibu Mkuu huyo alisema, umetokana na Wazimbabwe kutokubali kuwapa wapinzani nchi na pia ZANU-PF kusimamia vizuri sera ya uwekezaji.

“Tuna hakika tunapendwa na wazanzibabwe, hasa kutokana na serikali kuwa wa wazi na kuhakikisha inasimamia rasilimali za nchi na hata kusikiliza vilio vyao. Hivyo, ushindi wetu ni sauti ya Wazimbabwe,’’ alisema.

"Hata kelele zao  hasa za kuhoji kuwa Rais Mugabe ni mzee mwenye umri mkubwa, mbona wao wanasahau kuwa Malkia Elizabeth ni mzee kuliko hata nchi yenyewe ya Zimbabwe achilia mbali Rais Mugabe?, alisema na kuongeza;

“Malkia ni Mzee kuliko Zimbabwe yenyewe na bado ni malkia wa Uingereza. Hivyo Mugabe ni Rais wetu na bado wazimbabwe wanampenda".

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti na mwenyekiti wa Mkutano huo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana alisema miongoni mwa mambo ambayo Makatibu wakuu watajadili kwa kina ni namna ya kuwatafutia fursa vijana, ili waweze kushiriki katika masuala mbalimbali ya nchi zao ikiwemo kushika nafasi za uongozi.

Vyama vilivyoshiriki Mkutano huo, ni CCM (Tanzania), SWAPO cha Namibia, ZANU-PF cha Zimbabwe, MPLA cha Angola, FRELIMO cha Msumbiji na ANC cha Afrika Kusini.

0 Comments:

Post a Comment