HABARI

 

Tuesday, October 8, 2013

NAIBU KATIBU MKUU WA CHAMA CHA MAPINDUZI MH. MWIGULU NCHEMBA (MB) AUNGURUMA NCHINI UINGEREZA NA KUONYESHA UKOMAVU WAKE KIFIKRA.

0 Comments
· “Mabadiliko hayatakuja kwa kubadilisha vyama bali ni nia zenu {Mindset) zikifanywa kuwa mpya na mapenzi ya nchi yenu.” 

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Taifa na Mbunge wa Iramba Magharibi Mh. Mwigulu Lameck Nchemba akisisitiza Jambo katika hotuba yake aliyoitoa hapa nchini Uingereza iliyojaa mapenzi na Tanzania zaidi ya Itikadi na kupokelewa vyema na watanzania wengi hapa UK.

SOMA HABARI KAMILI
Katika hali iliyotajwa kuwa ni ya  furaha, kutokana na changamoto zilizokuwepo siku ya jumamosi jijini Leicester Uingereza, kijana shupavu na “JEMBE” la kujivunia katika Taifa la Tanzania Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa, na Mbunge wa Ilamba Magharibi Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba akiambatana na mshauri wa Rais mheshimiwa Rajabu Luhwavi, kwa pamoja waliweza kutoa majibu ya changamoto nyingi zinazolikabili Taifa kwa watanzania wengi waliojitokeza katika mkutano mkubwa uliohudhuriwa na watanzania wengi kutoka maeneo mbali mbali ya Uingereza.

Ujasiri, uwazi na ukweli wa mambo ya kiutendaji katika taifa letu ndio hasa imekuwa ni chachu na kivutio kikubwa kwa watanzania wengi waliohudhuria mkutano huo mkubwa jiji Leicester ambapo Mh. Mwigulu Nchemba aliweza kuweka wazi mengi ambayo serikali imeweza kuyafanya katika upande wa Elimu, Miundo mbinu na  huduma za afya kwa watanzania pia kutoa kasoro katika maeneo yanayokuwa vikwazo katika kutoa huduma bora.

“Nchi yetu ipo katika mchakato wa kupata katiba mpya, mojawapo ya mambo ambayo tunayafanyia kazi ni suala la uraia pacha. Ni pendekezo lililowakirishwa na Chama Cha Mapinduzi katika baraza zake za uchangiaji maoni ya Katiba mpya. CCM inawajali watanzania wote hivyo ikaona ni vyema na nyinyi mlioko ughaibuni kupata fursa sawa za kimaendeleo katika nchi yenu” alisema Mhe. Mwigulu Nchemba.

Mheshimiwa Nchemba aliendelea na kusema kwamba nchi yetu inapita katika kipindi cha mabadiliko. Idadi ya watanzania imeongezeka kwa kiasi kikubwa na wengi wa ongezeko hili ni vijana ambao ni watafutaji na wajasiliamali wengi. Kuna haja kubwa kama chama kubuni taratibu nzuri za kimaendeleo ili kuendana na wimbi hili la ongezeko la watu.

Mheshimiwa Nchemba kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi aliwasihi watanzania waishio Uingereza kutumia upeo (Exposure) waliyonayo katika kulisaidia taifa kupiga hatua zaidi za kimaendeleo kuliko kuwa na ushabiki wa siasa kama ilivyo kwa baadhi ya wanasiasa nyumbani na badala yake wawe chemichemi ya mawazo ya kimaendeleo katika nchi yao.

Watanzania mlioko nje mna nafasi kubwa ya kuchangia mawazo ya kujenga taifa lenu la Tanzania, nitawakilisha hoja yenu ya kupatiwa njia ya kuwakilisha mawazo yenu ama jambo lolote lenye busara na utendaji wa mabadiliko katika nchi yetu ya Tanzania ili pia mpate fursa ya kuwakilisha maoni na hoja za haja za kuleta mabadiliko. Kutokuwa na jukwaa lenu la kuwakilisha hoja zenu za kamandeleo ni kosa. Wazo lolote la kujenga  lazima liwakirishwe katika vikao rasmi kama mchango wa CCM diaspora, liongeza Mheshimiwa Nchemba.

Tengenezeni ajenda kulingana na ukomavu na upana wenu wa kimawazo ambao mnaupata katika nchi hizi za Magharibi ambazo zimepiga hatua kubwa za kimaendeleo kutokana na desturi zao za  kuthamini, kujituma na kutenda kazi zao kwa uadilifu mkubwa kwa mapenzi na nchi zao  ili kuchangia utekelezaji wa sera ya chama katika nchi yetu kwenye sekta mbalimbali za afya, elimu, miundombinu , sheria n.k. na mimi naahidi tutatengeneza na kuboresha uwanja mzuri wa mawasiliano kati yetu aliongeza Mheshimiwa Mwigulu Nchemba.

Mheshimiwa Nchemba pia alisisitiza upendo na umoja baina ya watanzania na kuwaomba wawe kitu kimoja na akawataka wana CCM Uingereza kuwa chachu ya kuwaunganisha watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa na vyama vyao. Mheshimiwa Nchemba pia amekuwa akikonga nyoyo za watanzania wengi kulingana na utashi na ufahamu wa kujibu maswali kiufasaha, wazi na kwa uhakika  pale alipoulizwa katika mikutano yake iliyofanyika katika majiji ya Leicester, Northampton na London nchini Uingereza.

Katika mkutano uliofanyika jijini Leicester watanzania wengi waliuliza maswali yanayohusu Katiba , Utawala wa Sheria wenye haki sawa kwa wote kama ilivyo katika nchi za kimagharibi, Uraia pacha, Kurugenzi inayoshughulikia masuala ya Diasprora ambayo badala ya kuwa kiunganishi imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa wanadiaspora kutokana huduma mbovu zenye kutokujali na majivuno kutoka kwa watendaji wake wakuu, Tunashauri watendaji katika kitengo hiki watokane na wanadiaspora wenyewe kwani upeo (exposure) wao kiutendaji utaleta ufanisi kuliko ilivyo sasa hivyo kuleta mchango wao kwa maendeleo ya Taifa. Pia Watanzania hao na wana CCM wameishauri serikali  kubadirisha taratibu zake za kiajira katika Balozi zetu za nje kwa kuwatumia watanzani wenyeji wa maeneo hayo ili kupunguza mzigo wa gharama serikali, kuongeza ufanisi kwani uelewa wa kufanya kazi katika mazingira wanayoishi wanaufahamu vyema zaidi kuliko kuleta watendaji wote katika Balozi zetu kutoka nyumbani.

Vilevile katika mkutano uliofanyika jijini Northampton siku ya Jumapili, mengi ya maswali yaliyoulizwa na watanzania waishio katika jiji hilo ni kama  katika masuala ya usalama wa nchi na raia wake dhidi ya matukio ya tindikali na majanga ya mabomu kule Arusha, tukio la kigaidi hivi karibuni nchini Kenya na utayari wa nchi yetu katika kukabiliana na wimbi kama hilo endapo litatokea nchini kwetu, mikakati ya kupambana na madawa ya kulevya pamoja na lile gonjwa sugu la rushwa.

Akijibu kwa ufasaha maswali hayo Mheshimiwa Rajab Luhwavi ambaye anaambatana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, katika ziara hii, alianza kwa kuwahakikishia usalama wa taifa Watanzania waliofika katika mkutano huo na kuwaondoa hofu hiyo. Na kuwajulisha kwamba serikali imeweka mikakati madhubuti ya kupambana na uhalifu wa aina hiyo na kwamba taratibu za lazima zinafanyika na hali ni shwari.

Imetumwa kwetu na: Abraham Sangiwa – Deputy Secretary Ideology and Publicity
Chama Cha Mapinduzi Uingereza (CCM UNITED KINGDOM)

Tarehe 08.10.2013.

0 Comments:

Post a Comment