HABARI

 

Saturday, September 8, 2012

MKUTANO WA ICGLR WAMALIZIKA NCHINI UGANDA

0 Comments
KAMPALA, UGANDA
Mkutnao maalumu wa  Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR),  kujadili hali ya usalama ya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), umemalizika mjini hapa, huku mawaziri wa ulinzi wa nchi wanachama wakipewa jukumu la kuangalia namna ya kuunda jeshi la pamoja kulinda mpaka kati ya DRC na Rwanda.

Rais Jakaya Kikwete, aliyehudhuria mkutano huo uliomalizika leo, alisema mapendekezo ya awali ya kamati ya mawazi saba wa ulinzi imekubaliwa na viongozi wa nchi za ICGLR na kwamba ili kutekelezwa wametakiwa kukaa na wenzao kutoka Sudan, Kenya, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Zambia,  maofisa wa majeshi na wa usalama.

Alisema viongozi wamekubaliana  jeshi hilo pia lilinde mpaka kati ya DRC na nchi zingine za Uganda na Burundi, ambapo mawaziri hao watajadili muundo wake na namna litakavyofanya kazi.

Waziri  wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na wenzake wa Rwanda, Uganda, DRC, Angola, Burundi na Congo Brazzaville, wamekuwa na mikutano kadhaa kuhusu suala hilo, kabla ya kuwasilisha taarifa kwenye mkutano wa viongozi hao uliofanyika jana. Walipewa jukumu hilo Julai, mwaka huu, katika mkutano wa viongozi wa ICGLR.

Rais alisema mapigano yaliyokuwa yakifanywa na kikundi cha waasi cha M23 hivi sasa yamesimama Mashariki mwa DRC, hivyo wamekubaliana mazungumzo yaendelee chini ya usimamizi wa Uganda, ambapo Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni, ndiye mwenyekiti wa ICGLR.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, wamekubaliana chombo cha ufuatiliaji wa makubaliano ya kumaliza mapigano DRC yaliyofikiwa Machi 23, 2009, ambacho kinaundwa na DRC na Rwanda, kiongezewe nguvu, hivyo kila mwanachama isipokuwa nchi hizo zenye wajumbe watatu, ziteue wajumbe wawili kila moja na ziwe zimetekeleza hilo ifikapo Septemba 14, mwaka huu.

Rais Kikwete alisema Tanzania imekwisha kutekeleza suala hilo na kwamba, mkutano mwingine wa ICGLR utafanyika mjini Kampala Oktoba 8, mwaka huu. Rais aliondoka jana jioni kurejea nyumbani.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, amesema anatarajia kuitisha mkutano kuzungumzia hali ya usalama Mashariki mwa DRC utakaofanyika mjini New York, Marekani, Septemba 27, mwaka huu.

Ban kupitia taarifa iliyotolewa jana katika mkutano wa ICGLR na Mwakilishi wake Maalumu na Kiongozi  wa UN katika Kanda ya Afrika ya Kati UNOCA), Abou Moussa, alisema mkutano huo utakaofanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa UN utatoa nafasi ya majadiliano yanayolenga kuongeza nguvu katika jitihada zinazofanywa na nchi za Maziwa Makuu katika kuupatia uvumbuzi mgogoro huo.
  
Alisema Mkuu wa Idara ya Oparesheni za Ulinzi wa Amani wa UN, Herve Ladsous, atazuru eneo la Maziwa Makuu kati ya leo na Septemba 15, mwaka huu, ikiwa ni maaandalizi ya mkutano huo. Aliwasihi viongozi wa nchi za ICGLR na jumuia ya kimataifa kushiriki, hususan kwa kuzingatia hali halisi ya Mashariki mwa DRC.

Ban alisema amani ya Mashariki mwa DRC ni muhimu, kwani inahatarisha usalama wa eneo la Maziwa Makuu na kwamba, mahitaji ya kibinadamu yanahitajika kwa kuwa takriban watu 226,000 hawana makazi Kaskazini mwa Kivu, huku zaidi ya watu 57,000 wamekimbilia Uganda na Rwanda.

Katibu Mkuu wa UN pia amerejea wito wake akionya wanaowasaidia waasi wa M23 na kuwataka waache. DRC imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kuwafadhili waasi hao, ambapo Rais wa Rwanda, Paul Kagame hakuhudhuria mkutano bali alituma mwakilishi, huku mwenzake wa DRC, Joseph Kabila alihudhuria.

0 Comments:

Post a Comment