HABARI

 

Monday, December 31, 2012

HOTUBA YA RAIS KIKWETE KUUKARIBISHA MWAKA MPYA WA 2013

1 Comments
Utangulizi 
Ndugu zangu, Watanzania Wenzangu;
Ni furaha na faraja kubwa kuifikia siku hii adhimu ya kuuaga mwaka wa 2012 na kuukaribisha mwaka 2013. Ni jambo la bahati ambayo hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuumaliza mwaka huu salama.  Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi ambao wangependa kuiona siku hii lakini hawakujaaliwa. Wametangulia mbele ya haki.  Tuendelee kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awape mapumziko mema.  Amin.   Nasi tumuombe Mola wetu atujaalie fanaka tele katika mwaka ujao.

Mapitio ya Mwaka 2012
Ndugu wananchi;
Mwaka tunaoumaliza leo ulikuwa wenye mambo mengi mazuri na mafanikio makubwa, lakini, pia, ulikuwa na changamoto zake. Baadhi zilikuwa ngumu na zipo zilizokuwa za kusikitisha na kuhuzunisha.
Ajali za barabarani na majini ziliendelea kupoteza maisha ya watu wengi na kusababisha majeraha na ulemavu kwa maelfu.  Ajali mbaya kuliko zote kutokea, mwaka huu, ilikuwa ile ya meli ya MV Skagit iliyotokea tarehe 18 Julai, 2012 ambapo watu 144 walipoteza maisha.  Ajali za barabarani zilizosababisha vifo nazo ziliongezeka kutoka 3,012 mwaka 2011 hadi kufikia 3,144 na kusababisha
vifo vya ndugu zetu 3,714.

Ndugu Wananchi;
  Kufuatia ajali ya MV Skagit ambayo ilitokea miezi 11 baada ya ile ya MV Spice Islander, Serikali zetu mbili zimekuwa zikishirikiana kwa karibu kuhusu masuala ya usafiri wa majini kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.  Kwa ajili hiyo SUMATRA na Zanzibar Maritime Authority zinafanya kazi kwa karibu zaidi na kanuni za usafirishaji wa abiria na mizigo na za usajili na ubora wa meli zimewianishwa.  Ni matumaini yetu kuwa hatua hizo zitasaidia kumaliza ajali zinazotokana na makosa ya wanadamu.

Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa ajali za barabarani tuliendelea na tutaendelea kuwahimiza madereva kuheshimu Sheria za Usalama Barabarani, waepuke uzembe na hasa ulevi wakati wa kuendesha.  Tutaendelea kuwakumbusha wenye magari kuhakikisha kuwa uzima wa magari yao unakuwa wa kiwango cha juu.  Hali kadhalika, tumewataka Polisi waongeze ukali na kuwabana ipasavyo madereva na wamiliki wa magari ili watekeleze wajibu wao na wasipofanya hivyo wawajibishwe inavyostahili.

                                        Hali ya Usalama
Ndugu wananchi;
Tunaumaliza mwaka huu nchi yetu ikiwa shwari, salama na tulivu.  Tuombe Mungu hali hii iendelee mwaka 2013 na idumu milele.  Mipaka ya nchi yetu ipo salama na uhusiano na majirani na nchi zote duniani ni mzuri.  Tunaendelea kutafuta suluhu ya mgogoro wa mpaka kati ya nchi yetu na Malawi katika Ziwa Nyasa kwa njia ya mazungumzo. Suala hilo limewasilishwa kwa pamoja na Serikali zote mbili kwa Mheshimiwa Joaquim Chissano, Mwenyekiti wa Umoja wa Viongozi Wastaafu wa Afrika kwa ajili kuzisaidia nchi zetu kupata ufumbuzi.  Matumaini yetu ni kuwa viongozi hao watalishughulikia suala hili mapema iwezekanavyo.
Ushirikiano wa Kanda

Ndugu Wananchi;
Ushirikiano wetu wa kikanda katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) unaendelea vizuri.  Mwaka huu nchi yetu imepewa heshima kubwa ya kuwa Mwenyekiti wa Chombo cha SADC kinachoshughulikia masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama.
  Jukumu hilo ni zito na hasa katika kipindi hiki ambapo kuna changamoto za kisiasa na kiusalama katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Madagascar na Zimbabwe.  Nchi yetu inatarajiwa kuongoza juhudi za kupata ufumbuzi wa migogoro hiyo migumu.  Ndiyo maana tulifanya Mkutano  Maalum wa Wakuu wa Nchi za SADC hapa Dar es Salaam tarehe 7 na 8 Desemba, 2012.  Mwaka ujao, kwa kushirikiana na wenzetu, tutaendeleza juhudi zetu.  Ni matumaini yangu kuwa tukipata ushirikiano wa viongozi na wananchi wa nchi husika na jumuiya ya kimataifa tutapata ufumbuzi tunaotaka.

Ndugu Wananchi;     
Kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, tumeendelea kushuhudia Jumuiya hiyo na harakati za utangamano zikizidi kustawi.  Jengo la Makao Makuu ya Jumuiya limekamilika na kuzinduliwa rasmi tarehe 28 Novemba, 2012.  Siku hiyo hiyo kule Athi River, Kenya, barabara ya kutoka Arusha hadi Athi River ilizinduliwa.  Barabara hii ni moja ya miradi kadhaa inayotekelezwa kwa pamoja na nchi wanachama wa Jumuiya wa Afrika Mashariki.

Mchakato wa utangamano wa kiuchumi wa Afrika Mashariki unaendelea kwa kasi.  Tanzania ikiwa sehemu kamili ya mchakato huo, lazima tuhakikishe kuwa tunakwenda nao sambamba.  Tusikubali kuachwa nyuma wala kuwa chanzo cha kuuchelewesha mchakato huo bila ya sababu za msingi.  Utangamano una maslahi kwa nchi yetu na manufaa yake ni makubwa.  Kwa mfano, mauzo yetu katika soka la Afrika Mashariki yameongezeka sana kutoka dola za Kimarekani milioni 58.6 mwaka 2000 hadi kufikia dola za Kimarekani milioni 409 mwaka 2011.

 Jumuiya imekuwa kichocheo muhimu cha kukuza uzalishaji, ajira na uchumi hapa nchini.  Kwa ukubwa wa nchi yetu na rasilimali tulizonazo tuna matumaini makubwa ya kunufaika zaidi siku za usoni.  Naweza kuthubutu hata kusema kuwa Tanzania inaweza kunufaika zaidi kuliko nchi nyingine wanachama wa Jumuiya hiyo.  Kinachotakiwa ni sisi kujipanga vizuri kwa sera na mipango ili tuzitumie fursa tulizonazo kwa maslahi ya uchumi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Tuache woga, tujiamini.

Matishio ya Usalama
Ndugu Wananchi;
Licha ya kumaliza mwaka nchi ikiwa shwari na yenye amani na utulivu, yalikuwepo matukio yaliyotishia usalama wetu.  Bahati mbaya na kwa masikitiko makubwa matukio hayo yalisababishwa na baadhi ya viongozi wa dini na siasa na wafuasi wao.  Kwa kweli kwa mara ya kwanza nchi yetu ilifikishwa kwenye hatari ya kutokea mgawanyiko mkubwa wa Watanzania au hata mapigano ya raia kwa misingi ya dini zao.  Bahati nzuri hilo halikutokea na Mungu aliepushe lisitokee kamwe.

Nimeshalisemea jambo hili siku za nyuma na napenda kurudia tena leo kuwasihi Watanzania wenzangu kupima athari za kauli zetu na matendo yetu kwa mustakabali wa jamii yetu, nchi yetu na watu wake.  Viongozi wa dini, waumini na viongozi wa siasa na wafuasi wao wanao wajibu maalum wa kuhakikisha kuwa Watanzania wanaendelea kuishi kwa upendo, amani na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini zao, makabila yao, rangi zao au maeneo watokako.  Hiyo ndiyo sifa ya nchi yetu tunayoijua sote ambayo ni njema na watu wengi wanataka kuja kujifunza kwetu na wale wenye shida wanatamani wawe kama sisi.  Hii ni tunu muhimu ya taifa ambayo tusikubali kuipoteza kwa maslahi binafsi ya watu wachache.

Ndugu Wananchi;
Wakati wo wote, lazima tutambue umuhimu wa kuvumiliana na kuheshimiana kwa tofauti zetu za kidini, rangi, kabila, tutokako na ufuasi wa vyama vya siasa.   Lazima pia tuhakikishe kuwa tunaheshimu sheria na taratibu zinazotawala mikutano na maandamano.   Tukiyazingatia hayo nchi yetu itakuwa haina tishio lo lote kwa amani na usalama wake.  Yasipozingatiwa tunaiweka nchi yetu hatarini.  Sisi katika Serikali tutakuwa hatuna la kufanya bali kutimiza wajibu wetu wa kulinda usalama wa raia na nchi yetu.  Wahusika watachukuliwa hatua na vyombo vya usalama na kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi.  Tulifanya hivyo mwaka huu na hatutakuwa na ajizi kufanya hivyo siku yo yote kama hapana budi.

Uhalifu Unapungua
Ndugu Wananchi;
  Inatia moyo kuona kuwa mwaka huu makosa ya jinai yalipungua na kufikia 66,255 yakilinganishwa na makosa 69,678 ya mwaka jana au 94,390 ya mwaka juzi.  Hii inathibitisha kuimarika kwa kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi wakishirikiana na wananchi na vyombo vingine vya usalama.  Pamoja na hayo lazima tuongeze juhudi za kupambana na uhalifu kwani bado matukio ni mengi mno na upungufu bado ni mdogo.  Tutaendeleza kazi tuifanyayo sasa ya kuliimarisha Jeshi la Polisi kwa rasilimali watu, zana na vitendea kazi husika.

Uhalifu wa Kimtandao
Ndugu Wananchi;
Tutaongeza nguvu katika kupambana na uhalifu unaoendeshwa na mitandao ya uhalifu ndani na nje ya nchi.  Mitandao hiyo hasa imekuwa inajihusisha na biashara ya kusafirisha wanadamu, biashara ya dawa za kulevya na biashara ya nyara za Serikali.

Mapambano dhidi ya uhalifu wa kimtandao yametuwezesha kukamata wahamiaji haramu 4,765 na tayari 1,611 wamerudishwa kwao.  Kwa upande wa dawa za kulevya watuhumiwa 6,929 walikamatwa mwaka huu ukilinganisha na 209 mwaka 2011. Kilo 55,285 za dawa za kulevya zilikamatwa mwaka huu ukilinganisha na kilo 17,752.4 mwaka jana.  Kwa upande wa nyara za Serikali, zilizokamatwa ni 1,416 na kati ya hizo 736 ni meno ya tembo.  Watuhumiwa 1,037 walikamatwa na kesi 746 zipo Mahakamani katika hatua mbalimbali.

Ndugu Wananchi;
Taarifa hizi zinathibitisha kuimarika kwa jitihada za kupambana na uhalifu wa kimtandao.  Tutaimarisha zaidi jitihada zetu mwaka 2013 ili tupate mafanikio zaidi.  Tutaviongezea uwezo wa rasilimali watu, zana, vifaa na fedha za uendeshaji vyombo vyetu vya usalama vinavyoongoza mapambano haya.

Tutaimarisha na kuendeleza ushirikiano baina ya nchi yetu na nchi jirani na nyinginezo duniani.  Hii itasaidia kutuongezea uwezo wa kupambana na mitandao ya uhalifu ndani ya nchi, kikanda na kimataifa.  Pia tutazipitia upya sheria za kupambana na makosa haya kwa nia ya kuziboresha.

Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2013, tutapanua na kuimarisha huduma ya matibabu kwa watu walioathirika na dawa za kulevya kote nchini.  Tutakamilisha ujenzi wa kituo cha Dodoma na kujenga kingine kipya Dar es Salaam.  Natoa wito kwa wale wote walioathirika au watu wenye watoto au rafiki au jamaa walioathirika waende hospitali kupatiwa matibabu kwani matibabu hayo ni bure.

Hali ya Uchumi
Ndugu wananchi;
Katika mwaka 2012, tunaoumaliza leo,  uchumi wa nchi yetu uliendelea kukua na kuimarika licha ya kuwepo kwa changamoto za upatikanaji wa umeme, kupanda kwa bei za mafuta na chakula duniani na uhaba wa mvua katika maeneo mengi nchini uliosababisha kupungua kwa uzalishaji na kupanda kwa bei za vyakula nchini.  Pia, licha ya kuendelea kwa msukosuko wa uchumi wa dunia na hasa katika Bara la Ulaya ambako ni soko kuu la bidhaa zetu na watalii.  Mategemeo yetu ni kuwa, mwaka huu, uchumi wetu utakua kwa asilimia 6.8 na  mwakani (2013) utakua kwa asilimia 7.0 ukilinganisha na asilimia 6.4 mwaka 2011.

Kwa jumla, ukilinganisha na makadirio ya IMF ya kiwango cha ukuaji wa uchumi wa dunia kuwa asilimia 3.3 mwaka huu, ni dhahiri kuwa uchumi wetu unakua kwa kasi nzuri na kuifanya Tanzania iendelee kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa.

Hali hii ya uchumi wetu ina maana kubwa mbili.  Kwanza, kwamba uchumi wetu umejenga uhimilivu dhidi ya misukosuko ya uchumi wa dunia.  Na pili, kwamba shughuli za uzalishaji na huduma zinazidi kukua na mauzo ya bidhaa ndani na nje ya nchi yameongezeka.  Kuongezeka kwa mauzo ya nje kumefanya akiba yetu ya fedha za kigeni kufikia dola za Marekani bilioni 3.9 mwezi Novemba, 2012 kiasi ambacho kinatuwezesha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi minne.

Ndugu Wananchi; 
Makusanyo ya mapato ya Serikali yatokanayo na kodi yalifikia shilingi bilioni 580.3 mwezi Oktoba, 2012 ikilinganishwa na shilingi bilioni 479.3 mwezi Oktoba 2011.  Matarajio yetu ni kufanya vizuri zaidi mwaka 2013 kwa mapato yatokanayo na kodi na yale yasiyotokana na kodi ambayo bado ni chini ya lengo.

Ndugu Wananchi;
Mfumuko wa bei kuwa juu ni changamoto ambayo tunaendelea kuikabili ili kuleta utulivu uliokamilifu kwa uchumi wetu na kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wa Tanzania.  Serikali imechukua hatua kadhaa kudhibiti hali hiyo na mafanikio ya kututia moyo yameanza kuonekana.  Kwa mfano, mfumuko wa bei umepungua kutoka asilimia 19.8 mwezi Desemba 2011 hadi asilimia 12.1 mwezi Novemba, 2012.  Kiwango hicho bado ni cha juu na hakikubaliki.  Tutaendelea kuchukua hatua zaidi ili tuweze kufikia lengo letu la mfumuko wa bei kuwa chini ya asilimia 10 ifikapo mwezi Juni, 2013.

Miongoni mwa mambo tuliyopanga kufanya ili kupunguza mfumuko wa bei ni kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme na kudhibiti mwenendo wa bei ya mafuta.  Kufanya hivyo kutasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na uchukuzi wa bidhaa. Aidha, tutaendelea kutekeleza mipango na mikakati ya kukuza na kuboresha kilimo nchini kwa lengo la kujihakikishia usalama wa chakula, kukuza pato la taifa na kupunguza umaskini hasa miongoni mwa wakulima.

Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo
Ndugu wananchi;
Mwaka huu tunaoumaliza leo ulikuwa na mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa utekelezaji wa miradi ya kuendeleza miundombinu nchini.  Tumeshuhudia miradi ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege, reli, bandari, umeme na maji ikikamilika, au kuanzwa au utekelezaji wake ukiwa unaendelea.  Hakika lengo la kuunganisha mikoa yote ya Tanzania Bara kwa barabara za lami siyo ndoto tena bali ni jambo la uhakika na litatimia muda si mrefu ujao.

Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa reli, mwaka huu tumeendelea kukarabati reli ya kati na kurejesha usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na Kigoma.  Mwaka ujao (2013) tutaendeleza kazi ya ukarabati wa reli hiyo muhimu na kuzidi kuboresha huduma.  Tumekamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege vya Mpanda na Songwe na tunaendelea kuboresha viwanja vya Tabora, Kigoma, Bukoba, Mafia, Mwanza na Zanzibar.  Tumeendelea kujenga na kupanua miundombinu ya maji nchini na kuboresha upatikanaji wa maji salama kwa Watanzania. Kwa mwaka huu usambazaji wa maji salama umefikia asilimia 87 kwa watu wa mijini na asilimia 61.5 vijijini.   Tutaendeleza kazi hiyo mwaka 2013.

Msongamano wa Magari Dar es Salaam
Ndugu Wananchi;
Katika Jiji la Dar es Salaam tumeendelea na tutaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza msongamano wa magari unaozidi kuongezeka.  Barabara mpya zimejengwa na zinaendelea kujengwa ndani na kuzunguka Jiji.  Barabara kadhaa zimepanuliwa na nyingine zitaendelea kupanuliwa.  Ujenzi wa miundombinu (barabara na vituo) ya mabasi yaendayo haraka umeanza.  Mwaka 2013 ujenzi wa barabara za juu ya nyingine katika makutano ya TAZARA utaanza na matayarisho ya kufanya hivyo kwa makutano ya Ubungo yatakamilishwa.
Tumetimiza ahadi yetu ya kutumia treni kusafirisha abiria katika jiji la Dar es Salaam.  Usafirishaji umeanza na unaendelea kati ya Stesheni na Ubungo na kutoka Stesheni ya TAZARA hadi Pugu – Mwakanga.  Mwaka ujao tutaendelea kuimarisha usafiri huo kwa kuongeza treni na idadi ya safari.  Tayari Mshauri Mwelekezi ameshateuliwa kufanya upembuzi yakinifu na kushauri kuhusu kupanua huduma hiyo mpaka ifike Tegeta, Bunju, Kimara, Luguruni, Kibaha, Mbagala-Rangi Tatu na Kongowe.  Ushauri huo pia utahusu kuwa na huduma bora ya usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam kwa maana ya aina ya njia, vichwa vya treni na mabehewa.  Tuliamua kuanza na reli na treni iliyopo, lakini nia yetu ni kufanya vile hasa inavyotakiwa iwe kwa usafiri wa treni mijini.
Umeme

Ndugu Wananchi;
Mwaka tunaoumaliza leo haukuwa rahisi kwa upande wa upatikanaji wa umeme.  Mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kidatu, Kihansi, Mtera, Pangani na Nyumba ya Mungu yameendelea kutokuwa na maji ya kutosha kwa sababu ya uhaba wa mvua.  Hivyo basi taifa limelazimika kutegemea umeme wa kukodi unaozalishwa kwa kutumia mafuta.  Umeme huo umekuwa wa gharama kubwa na hivyo kuwa mzigo mkubwa kwa TANESCO na taifa. Serikali imeendelea kushirikiana na TANESCO na kuisaidia kubeba mzigo huo.  Tutaendelea kufanya hivyo mwaka ujao na mpaka tutakapofikia hatua ya kutokuwa na ulazima wa kutumia umeme wa kukodi.

Ndugu Wananchi;
Mtakumbuka kuwa tulipopata tatizo la ukame na upungufu wa umeme mwaka 2006/2007, Serikali yetu iliazimia kuongeza uzalishaji wa umeme kutokana na vyanzo vingine vikiwemo gesi asili, makaa ya mawe, upepo na jua.  Nafurahi kusema kuwa, tangu wakati ule Serikali imeiwezesha TANESCO kujenga vituo vitatu vinavyozalisha MW 245 kwa kutumia gesi.

  Hatukuweza kuongeza zaidi uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi kwa sababu ya kiasi cha gesi kinacholetwa Dar es Salaam kutoka Songo Songo kuwa kidogo.  Ndiyo maana tukaamua kujenga bomba jipya kubwa la kusafirisha gesi kutoka Songo Songo hadi Dar es Salaam.

Ndugu Wananchi; 
Kwa nia ya kutaka kuhakikisha kuwa kutakuwa na gesi ya kutosha kuzalisha umeme mwingi zaidi pale inapohitajika, ikaamuliwa bomba hilo liendelezwe mpaka visima vya gesi vya Mtwara.  Ujenzi wa bomba hilo umeanza mwezi Novemba, 2012 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18.  Gesi itakayopatikana ina uwezo wa kuzalisha MW 3,000 za umeme.  Tayari mipango inaendelea ya kujenga mitambo ya kuzalisha MW 900 pale Kinyerezi ili mara gesi itakapofika umeme uzalishwe.  Hatua hiyo itatuwezesha kuung’oa mzizi wa fitina wa mgao wa umeme na mzigo wa kununua umeme ulio ghali.

Utafutaji wa Gesi
Ndugu Wananchi;
Tangu mwaka 2010 gesi nyingi imegundulika baharini na nchi kavu katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani. Utafutaji bado unaendelea na tuna matumaini kuwa gesi nyingi zaidi huenda ikagundulika.  Hivi sasa Serikali inaandaa sera na sheria mpya ya gesi ili kuboresha zinazotumika wakati huu.  Nia yetu ni kutaka kuhakikisha kuwa rasilimali hii adhimu inasimamiwa vizuri kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake pamoja na kulinda maslahi ya wawekezaji.

Napenda kutumia nafasi hii kuwahakikishia ndugu zetu wa kule gesi ilipogunduliwa au popote itakapogundulika, kuwa watanufaika sawia na katu hawatasahaulika.  Rai yao ya kutaka na wao wanufaike inakubalika na Serikali inajiandaa hivyo. Viongozi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa mfano, wanajua maelekezo niliyotoa kuhusu kuiandaa miji ya Mtwara na Lindi kupokea uchumi wa gesi.

Lakini, sharti la kutaka gesi isisafirishwe kwenda kokote na kwamba kila kitu kifanyike kwao halikubaliki. Rasilimali inayopatikana po pote katika nchi hii ni mali ya taifa zima na hutumika kwa manufaa ya taifa.  Katu siyo mali ya watu wa pale ilipogundulika au pale shughuli hizo zinapofanyika. Jumla ya makusanyo ya mapato yatokayo sehemu zote za nchi yetu na kutokana na vyanzo mbalimbali ndiyo yanayotumika kuhudumia watu wote po pote walipo.

Ndugu Wananchi;
 Huu ni msingi mzuri, ni sera nzuri na ni jambo jema la tunu, tulilorithi kwa waasisi wa Taifa letu, ambalo hatuna budi kulienzi na kulidumisha.  Nawasihi wanasiasa wenzangu tusiwaelekeze kwenye mambo mabaya wananchi tunaodai kuwapenda. Kutafuta umaarufu kwa agenda zinazopandikiza chuki kwa watu na kuligawa au kulibomoa taifa, ni upungufu mkubwa wa uongozi na uzalendo.  Tuache siasa za ubarakara na kuwapa watu matumaini yasiyotekelezeka.  Nawaomba wananchi msiwasikilize, si watu wanaowatakia mema na wala hawaitakii mema nchi yetu.

Elimu
Ndugu wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio katika utekelezaji wa sera yetu ya kupanua fursa ya elimu kwa Watanzania katika ngazi zote.  Mwaka huu vijana wetu wengi zaidi walijiunga na elimu ya msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu.  Hivi sasa tunaelekeza juhudi zetu zaidi katika kuongeza ubora wa elimu.    Kwa ajili hiyo, tumechukua hatua za makusudi za kupanua mafunzo na ajira za walimu wa shule za msingi na sekondari.  Kwa mfano,  mwaka huu walimu 24,621 wapya waliajiriwa kati yao 11,379 wa shule za msingi na 13,242 wa shule za sekondari.  Januari, 2013 tunategemea kuajiri walimu 28,746 kati yao 14,606 wa shule za msingi na 14,060 watakuwa wa shule za sekondari.
 Kwa sababu hiyo, uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi umeendelea kuwa mzuri.  Hivi sasa kwa shule za msingi uwiano umefikia 1:46 ukilinganisha na 1:56 mwaka 2005. Uwiano unaostahili ni 1:40. Kwa upande wa sekondari uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi hivi sasa ni 1:29 ukilinganisha na 1:20 unaostahili.  Kutokana na upanuzi wa vyuo vya kufundisha walimu nchini, bila ya shaka baada ya miaka mitatu hivi upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari haitakuwa kilio tena.

Ndugu Wananchi;
Upatikanaji wa vitabu nao unazidi kuwa bora.  Hivi sasa uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi ni 1:3 kwa shule ya msingi na sekondari 1:3 ukilinganisha na 1:5 kwa shule za msingi na sekondari 1:4 mwaka 2009.  Hata hivyo, tutaendelea kuongeza mgao wa fedha katika bajeti ya elimu ili kuongeza upatikanaji wa vitabu na vifaa vingine vya kusomea na kufundishia.  Tunataka katika muda mfupi ujao uwiano uwe 1:1.

Kwa upande wa maabara za sayansi, tarehe 4 Novemba, 2012, nilipokuwa kwenye ziara ya Mkoa wa Singida, nilitoa agizo la kutaka ndani ya miaka miwili, kuanzia mwaka 2013, kila shule ya sekondari ya kata nchini iwe na majengo ya maabara yaliyokamilika.  Yawe pia yanatumika kwa maana ya vifaa na mahitaji muhimu.  Nimewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa agizo hili linatekelezwa kwa ukamilifu.  Kuanzia sasa, katika ziara zitakazofanywa Mikoani na mimi, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu tutapenda kupata taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wake.

Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa ufundishaji imedhihirika kwamba mkakati maalum unahitajika kuboresha ufundishaji wa masomo ya hisabati, kiingereza na sayansi katika shule za msingi na sekondari.  Matokeo ya mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne kwa miaka mingi sasa yanathibitisha haja hii.  Sasa wakati umefika kwa suala hili kulipa uzito unaostahili.  Tutafanya hivyo kuanzia mwaka 2013.
Afya
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2012 ulikuwa na mafanikio mengi ya kutia moyo kwa upande wa sekta ya afya nchini pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali. Kazi ya kusogeza huduma ya afya karibu na wanapoishi watu kwa maana ya kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali mpya na kuimarisha zilizopo iliendelea kutekelezwa kwa mafanikio kote nchini.

Hali kadhalika, uwezo wetu wa ndani wa uchunguzi na tiba ya magonjwa makubwa umezidi kuimarika mwaka huu. Upatikanaji wa dawa, vifaa vya uchunguzi na vifaa tiba umeendelea kuboreshwa.  Aidha, mafunzo na ajira za madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa afya vimeendelea kuongezwa.  Kituo cha Tiba ya Maradhi ya Moyo kimekamilika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mwaka ujao (2013) shughuli za upasuaji na nyinginezo husika kutibu maradhi ya moyo zitakuwa zimeboreshwa sana.  Upanuzi mkubwa wa Hospitali ya Saratani ya Ocean Road umekamilika.  Kwa ajili hiyo, huduma zitakuwa bora zaidi na msongamano wa wagonjwa hospitalini hapo utakuwa umemalizika.  Ujenzi wa hospitali kubwa ya kisasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma unaendelea vizuri na inatarajiwa kukamilika mwaka 2014.  Hospitali hiyo itatumika kufundishia wanafunzi wa udaktari na uuguzi.

Ndugu Wananchi;
  Mwaka huu pia, tumekamilisha matayarisho ya kuanza ujenzi wa hospitali kubwa na ya kisasa kabisa kule Mlonganzila, Dar es Salaam.  Ujenzi utaanza Februari 2013 na kukamilika Februari, 2015.  Hospitali hii pia itakuwa ya kufundishia wakati Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili kitakapohamishia sehemu kubwa ya shughuli zake huko Mloganzila.  Mchakato wa ujenzi wa Chuo hicho nao unakaribia kuanza.  Kuwepo kwa hospitali hizi kutaongeza sana uwezo wetu wa ndani wa uchunguzi na tiba.  Sasa naweza kuthubutu kusema kuwa safari ya kupunguza wagonjwa tunawaopeleka nje tumeianza  kwa dhati.

Ndugu Wananchi;
 Tumeendelea kupata mafanikio katika mapambano dhidi ya magonjwa makubwa yanayosababisha vifo vingi kama vile UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria.  Maambukizi na vifo vinazidi kupungua.   Pia vifo vya kina mama na watoto vinaendelea kupungua.

Kwa mujibu wa taarifa za mwaka huu za Shirika la Afya Duniani, vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano hapa Tanzania vimepungua kutoka vifo 81 kwa kila watoto 1000 waliozaliwa hai mwaka 2009 hadi kufika vifo 65.2 mwaka 2011 na vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 51 kwa kila watoto 1000 waliozaliwa hai mwaka 2009 na kufikia vifo 45 mwaka 2011. Mafanikio haya yanaiweka Tanzania katika orodha ya nchi 10 zinazofanya vizuri duniani katika kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Ndugu Wananchi;
   Hatuna budi kufahamu kuwa haya ni matokeo ya kufanya vizuri kwenye chanjo kwa watoto ambayo imefikia wastani wa asilimia 90.  Pia imechangiwa na mafanikio yetu katika kupunguza maambukizi ya malaria na UKIMWI kwa watoto.  Naamini tutapata mafanikio makubwa zaidi kuanzia mwaka 2013 tutakapoanza chanjo dhidi ya kichomi (pneumonia) na ugonjwa wa kuharisha kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.  Aidha, tukiendelea kutekeleza kwa dhati mpango wa kila mtoto kulala kwenye chandarua kilichotiwa dawa na ule Mpango Kabambe wa Kuzuia Maambukizi ya Mama Kwenda kwa Mtoto niliouzindua kule Lindi tarehe 1 Desemba, 2012, mambo yatakuwa vizuri zaidi.
  
Sensa ya Watu na Makazi
Ndugu wananchi;
Leo asubuhi kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja nilitangaza matokea ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwezi Agosti, mwaka 2012.  Matokeo haya yanaonyesha kwamba idadi ya watu nchini Tanzania ni milioni 44,929,002 kati yao watu milioni 43,625,434 wanaishi Tanzania Bara na milioni 1,303,568 wanaishi Zanzibar.  Ukilinganisha na Sensa ya mwaka 2002 tulipokuwa na watu milioni 34.4, hili ni ongezeko la watu milioni 10.5 au wastani wa asilimia 2.6 kwa mwaka.
Matokeo haya yana maana kubwa kwa Serikali na kwa kila mmoja wetu.  Kwa kasi hii ya ongezeko la watu ifikapo mwaka 2016 Tanzania itakuwa na watu milioni 51.6.  Hii ni idadi kubwa sana ya watu inayoleta changamoto kwa Serikali na jamii.  Hatuna budi kutambua maana ya idadi hiyo ya watu na kujipanga vyema kukidhi mahitaji yao na hasa kuhakikisha kuwa maskini hawaongezeki na huduma zinatosheleza mahitaji na zina ubora wa juu.  Kazi hiyo lazima ianze sasa na ionekane katika Mipango ya Maendeleo.

Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu, sisi wananchi, taarifa hii inamlazimu kila mmoja wetu atambue kuwa kwa kasi hii, siku za usoni nchi yetu itakuwa na watu wengi, hivyo ushindani kwa rasilimali utakuwa mkubwa.  Watakaofanikiwa wakati huo ni wale wenye familia ndogo au zile ambazo zimepanga uzazi.  Tukipanga uzazi tunajipa nafasi ya kutunza na kulea vizuri watoto wetu na kuwapatia mahitaji yao muhimu ya maisha.

Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kurudia kuwashukuru wananchi wenzangu wote kwa ushirikiano wenu uliowezesha zoezi zima kufanikiwa kiasi hiki.  Aidha, nawashukuru kwa dhati viongozi, watendaji wakuu na maofisa wote waliopanga, kuratibu, kusimamia na kutekeleza zoezi la kuhesabu watu.  Natoa shukrani maalum kwa Kamati ya Kitaifa ya Sensa, Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Jamhuri ya Muungano na Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar na makarani wote wa sensa.  Penye nia pana njia.  Tumeweza kushinda changamoto zote na kuwapatia Watanzania nyenzo muhimu ya kupanga mipango ya maendeleo yao.

Vitambulisho vya Taifa
Ndugu wananchi;
Mwaka huu tumeanza zoezi la kusajili watu na makazi kwa ajili ya kuandaa kutoa Vitambulisho vya Taifa kuanzia mwaka 2013.   Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ilifanya zoezi la majaribio katika mkoa wa Dar es Salaam na wilaya ya Kilombero ambalo lilifanikiwa.  Hivi sasa wanaendelea na zoezi hilo Zanzibar. Maandalizi kwa ajili ya kutekeleza zoezi la kutoa vitambulisho nchi nzima kuanzia mwaka 2013 yanakwenda vizuri.   Napenda kuwasihi wananchi wenzangu wakati utakapofika kutoa ushirikiano unaostahili kwa maafisa watakaohusika na kukusanya taarifa na kutoa vitambulisho ili zoezi lifanikiwe ipasavyo.  Nawaomba muitumie vizuri fursa hii ya kujisajili na kupata vitambulisho.

Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu wananchi;
Mtakumbuka kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nililiyoiunda tarehe 1 Mei, 2012 ilianza kazi yake rasmi tarehe 29 Juni, 2012 na inaendelea vyema.  Mpaka sasa Tume imekamilisha hatua ya kwanza ya kukusanya maoni ya mtu mmoja mmoja katika Mikoa yote nchini.  Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kutoa maoni.  Zoezi linalofuata ni la kukusanya maoni ya makundi maalumu kuanzia mwezi  Januari, 2013.  Natoa wito kwa makundi hayo nayo kushiriki vizuri kwenye hatua hii muhimu.  Baada ya hatua hiyo kukamilika, Tume itaandaa Rasimu ya Katiba ambayo wanategemea itakuwa tayari mwezi Mei, 2013.

Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume, rasimu hiyo itawasilishwa kwenye Vikao vya Mabaraza ya Katiba vitakavyofanyika kati ya mwezi Juni na Agosti, 2013.    Tume itatangaza muundo na namna ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza hayo na utaratibu utakaotumika wakati wa kujadili na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba wakati huo ukiwadia.

Baada ya kukamilika kwa Vikao vya Mabaraza ya Katiba, Tume itakamilisha Rasimu ya Katiba ambayo itachapishwa kwenye Gazeti la Serikali kama yalivyo matakwa ya Sheria.  Aidha, itachapishwa katika magazeti ya kawaida kwa wananchi kusoma.  Mwezi Novemba, 2013 rasimu hiyo itawasilishwa kwenye Bunge Maalum kujadiliwa na kupitishwa.  Baada ya Bunge Maalum kupitisha Rasimu ya Katiba, Rasimu hiyo itapelekwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni.

Ndugu Wananchi;
   Matarajio yetu ni kwamba kama kila kitu kitakwenda kama inavyotarajiwa nchi yetu itakuwa na Katiba Mpya iliyotokana na maoni na matakwa ya wananchi ifikapo mwaka 2014.  Mwaka huo Muungano wetu utakuwa unatimiza miaka 50 hivyo hiyo itakuwa zawadi ya tunu kubwa.  Tukifanikiwa kupata Katiba mpya wakati huo, tutafanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kutumia Katiba hiyo.  Inshallah, Mwenyezi Mungu atajaalia baraka zake, nia yetu njema itatimia.  Pamoja na hayo, natoa wito kwenu wananchi wenzangu kushiriki kwa ukamilifu katika hatua zote za mchakato ili tuweze kujenga muafaka kuhusu Katiba tunayoitaka.

Marekebisho ya Sheria
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Februari, 2012, nilieleza kwamba katika mazungumzo baina ya Serikali na  vyama vya siasa na wadau wengine juu ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tulikubaliana tushughulikie marekebisho ya Sheria hiyo hatua kwa hatua.   Tulikubaliana kuanza na mambo yanayohusu Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi ili Tume iundwe na ianze kazi.  Baada ya hapo tuangalie vipengele vinavyohusu Bunge Maalum na Kura ya Maoni.  

Tulifanya hivyo kuhusu Tume ya Katiba na sasa tunajiandaa kuanza mazungumzo kuhusu ngwe iliyobaki yaani, Bunge Maalum na Kura ya Maoni.  Kama mazungumzo yatakamilika mapema kunako Januari, 2013 mapendekezo hayo yatafikishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano katika kikao cha Februari   kwa uamuzi.  Vinginevyo itakuwa katika Bunge la Aprili, 2013

Ndugu Wananchi;
Kuhusu Kura ya Maoni, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaelekeza kuwa Kura ya Maoni itatungiwa Sheria yake maalum.  Ni matumaini yangu kuwa matayarisho yake yataanza mapema iwezekanavyo.  Nawasihi wananchi wenzangu, viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kijamii tuwe watulivu, tuendelee kushirikiana katika mchakato huu wa Katiba mpaka tulifikishe jahazi ufukweni salama kwa mustakabali mwema wa nchi yetu na watu wake.

Mfumo wa Dijitali
Ndugu wananchi;
Bila ya shaka mtakumbuka taarifa za Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Tume ya Mawasiliano kwamba kuanzia tarehe 1 Januari, 2013 nchi yetu itahamia katika mfumo wa mawasiliano unaotumia teknolojia ya dijitali (au kidijiti kwa tafsiri ya BAKITA) badala ya huu wa sasa wa analojia. Uamuzi huu unakuja kufuatia uamuzi wa kimataifa kwamba nchi zote duniani ziwe zimeingia kwenye mfumo huu ifikapo mwaka 2015.  Pia unazingatia uamuzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa nchi zetu kuanza safari hiyo tarehe 1 Januari, 2013.

  Hapa nchini zoezi hili litafanyika kwa awamu.  Litaanza katika mikoa saba ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mbeya, Kilimanjaro, Mwanza na Tanga na mingine itafuata kwa mujibu wa ratiba itakayopangwa.

Ndugu Wananchi;
 Teknolojia ya dijitali katika mfumo wa mawasiliano hufanya picha za televisheni kuwa nzuri na hazina chenga chenga.  Mawasiliano ya simu yatakuwa mazuri zaidi.  Vile vile, itakuwa rahisi kupata huduma za televisheni kwenye simu za mkononi na huduma ya intaneti kwenye televisheni.

Ndugu Wananchi;
Ili kuweza kutumia teknolojia hii, kila televisheni inatakiwa iwe na kifaa kiitwacho king’amuzi. Vifaa hivi vipo kwa wingi madukani na wengine tayari wanavyo. Naomba niwatoe hofu kwamba kwa kuingia katika mfumo huu siyo lazima kununua televisheni mpya. Televisheni yo yote yenye vitundu vitatu vya rangi za njano, nyeupe na nyekundu itaweza kufanya kazi kwenye mfumo wa dijitali. Hata wale ambao hawana televisheni za namna hiyo wanaweza kununua kifaa cha kuunganishia king’amuzi na mambo yakawa mazuri.

Uhusiano wa Kimataifa
Ndugu wananchi;
Katika mwaka 2012, uhusiano wetu na washirika wetu wa maendeleo ulikuwa mzuri na uliendelea kuimarika.  Wote wanaridhika na kusifu kazi nzuri inayofanywa na Serikali yetu na ndiyo maana wanaendelea kushirikiana nasi na kutoa misaada ya maendeleo.  Aidha, wameonesha nia thabiti ya kuendelea kushirikiana nasi na kutusaidia katika harakati zetu za kujiletea maendeleo.

Napenda kutumia nafasi hii kwa niaba yenu nyote kutoa shukrani za dhati kwa washirika wetu wa maendeleo kwa mchango mkubwa wanaoendelea kutoa kwa maendeleo ya nchi yetu.  Nawahakikishia kuwa tunathamini sana ushirikiano wao na misaada yao na tutafanya kila tuwezalo kudumisha ushirikiano baina yetu.

Mkutano wa Smart Parntership
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu nchi yetu ilipata bahati ya kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kikanda na kimataifa.  Mikutano hiyo ni pamoja na Mkutano Mkuu wa Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mkutano Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Chanjo (GAVI) na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za  SADC.

Bahati nzuri mwaka 2013 Tanzania itakuwa mwenyeji wa mikutano mingine ukiwemo ule wa Global 2013 Smart Partnership Dialogue utakaofanyika Dar es Salaam kuanzia tarehe 24 – 28 Mei, 2013.  Huu ni mkutano unaohusisha nchi nyingi duniani na kutoka takriban mabara yote.  Mkutano huu hukutanisha na kushirikisha viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa sekta binafsi wakiwemo wa makampuni makubwa ya kimataifa, wasomi  na wawakilishi wa asasi za kiraia na watu binafsi.

Kwa kawaida katika mkutano kama huu huwepo agenda maalum, aghalabu kuhusu masuala ya uchumi, biashara na maendeleo.   Mkutano wa mwaka 2013 utazungumzia “Matumizi ya Sayansi na Teknolojia kwa Ajili ya Maendeleo ya Afrika” (Leveraging Science and Technology for Africa’s Development).  Kwa kweli ni kipaumbele muafaka kabisa, ndiyo maana na sisi tumefarijika kuukaribisha.

Ndugu Wananchi;
Kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huu wa watu zaidi ya 500 mashuhuri, ni heshima kubwa kwa nchi yetu.  Ni nafasi nzuri ya kuitangaza Tanzania na fursa zake za uwekezaji, biashara na utalii. Pia, ni nafasi nzuri kwa wafanyabiashara wetu kutangaza shughuli zao na fursa za biashara na uwekezaji wanazotaka kushirikisha wafanyabiashara wa nje.  Naomba tuitumie vyema fursa hiyo adimu kwa manufaa ya taifa na ya waanyabiashara wetu.   Tuwaonyeshe wageni wetu upendo na ukarimu kama ilivyo sifa yetu Watanzania ili waondoke na kumbukumbu nzuri za nchi yetu na watamani kurudi tena kutembea au kuwekeza.
 
Hitimisho
Ndugu wananchi;
Tunatarajia kuwa mwaka 2013 utakuwa mwaka wa mafanikio makubwa zaidi katika nyanja zote kuzidi mwaka 2012.  Mambo yaliyokwama mwaka 2012 yatakwamuliwa.   Ajira zitaongezeka kwa uwekezaji vitega uchumi kuongezeka na kuwajengea uwezo wajasiriamali wazalendo, ili waweze kujiajiri wenyewe na kuajiri wengine.  Kwa ajili hiyo, Mifuko ya kusaidia wajasiriamali wadogo, wanawake na vijana itafufuliwa na kutengewa fedha nyingi katika bajeti ya Serikali.
 Mwaka 2013 ni mwaka wa matumaini, hivyo kila mmoja wetu anatakiwa kujituma na kutimiza wajibu wake.  Maisha bora yatakuja kwa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake ipasavyo.  Kama kila mtu atafanya kazi kwa bidii na maarifa, na, kama kila mmoja wetu atajivunia matokeo ya kazi yake na siyo uhodari wa maneno yake ya uchambuzi wa hali.  Kila mtu achukie uvivu na tabia ya kulalamika pasipo kufanya kazi.

Ndugu Wananchi;
Mimi na wenzangu Serikalini tunawaahidi ushirikiano wa hali ya juu na kwamba tutawatumikia kwa moyo wetu wote, kwa nguvu zetu zote na kwa maarifa yetu yote.  Tunataka kukidhi matarajio na imani ya wananchi kwa Serikali yao. Tutaendelea kuimarisha utendaji kazi Serikalini na kuhimiza uwajibikaji katika ngazi zote za uongozi. Tutaendeleza mapambano dhidi ya rushwa bila ajizi na watumishi wasio waaminifu, wazembe, wabadhirifu wa mali ya umma watawajibishwa ipasavyo.  Wananchi pia wanao wajibu wa kuwa raia wema na wazalendo wa kweli kwa nchi yao. Kila mmoja wetu ajiulize ataifanyia nini jamii yake na nchi yake badala ya kuuliza itamfanyia nini.

Ndugu zangu,Watanzania Wenzangu;
Nawatakieni nyote heri na fanaka tele katika mwaka mpya wa 2013. Tusherehekee pamoja kwa amani na utulivu.

Mungu Ibariki Afrika!
   Mungu Ibariki Tanzania!
        Asanteni sana kwa kunisikiliza.                                                                                                                                                                                                                                                                          
Read more...

Sunday, December 30, 2012

MWENYEKITI WA CHADEMA AMTANGAZA DK. SLAA KUWA MGOMBEA URAIS WA CHADEMA 2015

0 Comments

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza kuwa Katibu Mkuu wake, Dk Willbrod Slaa atapewa fursa ya kuwania nafasi ya Urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, mwaka 2015. 

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza hatua hiyo jana, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mpira, mjini Karatu mkoani Arusha, huku yeye akijiweka kando kuwania nafasi hiyo.

Hata hivyo, Dk Slaa mwenyewe alipoulizwa iwapo ana nia ya kugombea urais mwaka 2015, alisema: “Kwani mwaka 2010 nilijitangaza mwenyewe?, Iwapo wanachama wa Chadema watanipendekeza, nitafikiria kufanya hivyo.”

Katika maelezo yake Mbowe alisema: “Kama Mwenyezi Mungu atampa uhai na afya njema hadi mwaka 2015, Dk Slaa anatosha na Chadema, tutampa fursa nyingine ya kupeperusha bendera ya chama kwenye nafasi ya urais.” 

Huku akishangiliwa na umati wa wana chama wa Chadema Mbowe aliongeza: “Ninataka wanaotumia ugombea Urais kama kete ya kuleta mtafaruku ndani ya Chadema watambue hivyo.” 

Alibainisha kuwa, binafsi hana nia ya kuwania urais na badala yake atatumia nguvu, uwezo na kila kilicho ndani ya uwezo wake, kukijenga Chadema ili kushinde uchaguzi na kushika dola. 

Mbowe alisema kwa muda mrefu kumekuwapo mbinu na jitihada za kumgombanisha yeye na Dk Slaa kuhusu nafasi ya urais na kutamba kwamba njama hizo kamwe hazitafanikiwa. Mwenyekiti huyo wa Chadema alitumia pia mkutano huo kutangaza kumalizika kwa mgogoro uliokuwapo kati ya viongozi wa chama hicho wilayani Karatu. 

Hata hivyo, awali katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Mbowe alisema: “ Kikao cha CC (Kamati Kuu), kitakachofanyika Januari mwakani ndicho kitakachoweka utaratibu rasmi wa watu wanaotaka kuwania kiti cha udiwani, ubunge na urais mwaka 2015 na kutangaza nia zao na vigezo vya uteuzi.” 

Alisema chama hicho kinakusudia kuwapa nafasi wenye nia kujitokeza mapema, ili kutoa fursa ya kuwaelewa, kuwaandaa, kuwapa mafunzo, kuwaeleza majukumu na wajibu wao, kuwaeleza sera, misimamo na malengo ya chama hicho.

Mbowe alisema kuwa mpango huo utakihakikishia Chadema wagombea wenye uwezo na uhakika wa kushinda mwaka 2015. “Nia ya mpango huu ni kuepuka watu wanaodandia kuomba uteuzi wa kugombea dakika za mwisho,” alisema Mbowe.

Aliweka wazi kuwa chama hicho kitakuwa makini katika uteuzi wa nafasi ya urais kwa sababu ni nafasi nyeti, isiyohitaji kujaribu wala mzaha. 

Alisema kwamba chama hicho hakitasubiri wala kupokea waliokosa fursa za uteuzi katika vyama vingine, kikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao wanaokimbilia Chadema dakika za mwisho akisema kuwa uzoefu umeonyesha wengi wao wanaendelea kuwa mamluki.

Mwananchi 
Read more...

Friday, December 21, 2012

MAHAKAMA YA RUFANI YAMREJESHEA UBUNGE LEMA

0 Comments

 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (katikati) akiwa katika mahakama ya rufaa wakati wa hukumu ya rufaa ya mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema leo
 Wakili wa Godbless lema, Tundu Lissu (katikati)
Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema akilakiwa na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kushinda rufaa yake ya kupinga kuvuliwa ubunge wa Arusha mjini katika Mahakama ya Rufaa jijini Dar es Salaam. 
 Wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakiongozwa na mbunge wa Arushja Mjini, Godbless Lema kuelekea makao makuu ya chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam
 Wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakiongozwa na mbunge wa Arushja Mjini, Godbless Lema kuelekea makao makuu ya chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam
 Wakili wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Tundu Lissu akizungumza na wafuasi wa chama hicho makao makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam
 Mbunge wa Ubungo John Mnyika akizungumza na wafuasi wa Chadema makao makuu ya chama hicho leo
 Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe akizungumza na wanachama wa chama hicho waliokusanyika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam jana baada ya mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema kushinda rufaa yake ya kupinga kuvuliwa ubunge katika jimbo hilo.
 Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema  akizungumza na wafuasi wa chama hicho waliokusanyika makao makuu ya chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam
Dk. Slaa akizungumza
Read more...

Friday, December 14, 2012

RAIS WA MADAGASCAR AKUTANA NA RAIS KIKWETE, IKULU

0 Comments

Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina ambaye amewasili mjini Dar es Salaam mchana wa leo, Ijumaa, Desemba 14 kwa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini. Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Rajoelina, amelakiwa  na mwenyeji wake,  Rais Jakaya Mrisho Kikwete, na kuwa na mazungumzo, Ikulu.
   Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo amepewa jukumu na viongozi wenzake ndani ya Jumuiya hiyo kukutana na viongozi wa Madagascar kuwaelezea maamuzi ya mkutano wa viongozi  wa SADC uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini Dar es Salaam. Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, mwanzoni mwa wiki hii, Mheshimiwa Ravalomanana alithibitisha kuwa amekubaliana na maamuzi ya viongozi wa SADC. 
    Miongoni mwa mambo mengine, viongozi hao wa SADC wanataka viongozi hao wawili wa Madagascar washawishiwe na wakubali kutogombea katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika nchini humo mwakani. Pichani, Rais Kikwete akiwa na mgeni wake, Ikulu (PICHA NA IKULU
Read more...

Sunday, December 9, 2012

MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA KUJITOLEA SERIKALI YATANGAZA KUTENGA BILIONI 1.5 KUSAIDIA VIJANA

0 Comments

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini (UNDP) Bw. Phillippe Poinsot akifungua rasmi Siku ya Kimataifa ya Kujitolea bila malipo kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Disemba ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Volunteer Action Counts’.(Picha na www.dewjiblog.com)

Mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kujitolea Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Bi. Venerose Mtenga akihutubia na kuwaasa vijana kufanya kazi kwa kujitolea bila kusubiri malipo.
Mgeni rasmi amewaasa vijana kuwa tayari kufanya kazi kwa kujitolea kwa sababu Serikali kupitia Wizara yake imetenga Bilioni 1.5 kwenye mfuko Maalaum wa Vijana ili kuwakopesha vijana kwenye vikundi vidogo vidogo ili wajiunge na ujasiriamali na kujitoa katika umaskini.

Mshehereshaji wa Siku ya Kimataifa ya kujitolea Austin Makani akijadiliana na washiriki kuhusiana na umuhimu wa vijana kujitolea.

Kutoka kushoto ni Mgeni rasmi Bi. Venerose Mtenga, Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Bw. Phillippe Poinsot na Afisa Program wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kujitole (UNV) Bi. Stella Karegyesa wakifuatilia program zilizokuwa zikiendelea wakati wa maadhimisho hayo.

Pichani Juu na Chini baadhi ya wanafunzi wa vyuo mbalimbali, wanachama wa UN Clubs na wageni waalikwa waliohudhuria maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya kujitolea.

Baadhi ya washiriki wakijadiliana umuhimu wa kujitolea katika makundi.

Mgeni rasmi Bi. Venerose Mtenga na Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Bw. Phillippe Poinsot wakitoka ukumbi.

Mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kujitolea Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Bi. Venerose Mtenga, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini (UNDP) Bw. Phillippe Poinsot na Afisa Program wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kujitole (UNV) Bi. Stella Karegyesa katika picha ya pamoja na washiriki.
Read more...

Saturday, December 8, 2012

VIONGOZI WA SADC WAFANYA KIKAO CHA DHARURA LEO JIJINI DAR ES SALAAM

0 Comments


Rais Jakaya Kikwete, akikaribisha viongozi wenzie wa nchi za SADC katika  kikao cha dharura cha Jumuiya hiyo katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam leo Desemba 8, 2012

Rais Jakaya Kikwete, Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini, Rais Hifikepunye Pohamba wa Namibia na Katibu Mkuu wa SADC Dk.Tomaz Salomao pamoja na Mawaziri wa nchi hizo wakipitia rasimu ya muhtasari wa kikao kabla ya kuanza kwa kikao cha dharura cha Jumuiya hiyo katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam leo Desemba 8, 2012
 Rais Jakaya Kikwete, katika picha ya pamoja na  viongozi wenzie wa nchi za SADC katika  kikao cha dharura cha Jumuiya hiyo katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam leo Desemba 8, 2012. PICHA ZOTE NA IKULU, DAR ES SALAAM,TANZANIA.
Read more...

Sunday, November 11, 2012

HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CCM KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA NANE WA CHAMA CHA MAPINDUZI, UKUMBI WA KIZOTA – DODOMA, TAREHE 11 NOVEMBA, 2012

0 Comments

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amefungua Mkutanbo Mkuu wa Nane wa CCM, kwa kutoa hotuba  ambayo wengi wameielezea kuwa ni nzito kutokana na kupambanua na kutoa maelekezo ya nini kifanyike na kuzingatiwa zaidi kwa ajili ya ustawi wa Tanzania na Chama Cha Mapinduzi.

Ifuatayo ni Hotuba kamili Kama ilivyosomwa na  Rais Kikwete kwenye ukumbi wa Kizota, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Utangulizi

Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais Mstaafu wa Zanzibar;
Ndugu Pius Msekwa, Makamu Mwenykiti wa CCM wa Bara;
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Ndugu Benjamin William Mkapa;
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Waziri Mkuu;
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Wilson Mukama;
Ndugu  Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM;
Wageni wetu waalikwa kutoka vyama rafiki,
 Ndugu zetu wa Vyama vya Siasa Nchini;
Waheshimiwa Mabalozi,
Viongozi wa Dini,
 Wageni Waalikwa,
 Mabibi na Mabwana;


Kama ilivyo ada, naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa Dodoma, siku ya leo, kwenye Mkutano Mkuu wa Nane wa Chama cha Mapinduzi.
Ndugu Wajumbe;
Karibuni Dodoma.  Karibuni Mkutanoni.  Nawapeni pole kwa safari.  Tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika salama na tuombe turejee makwetu salama. Kwa niaba yenu, niruhusuni niwashukuru wenyeji wetu, yaani wana-CCM na wananchi wote wa Dodoma, wakiongozwa na Alhaji Adam Kimbisa, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa Dkt. Rehema Nchimbi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.  Tunawashukuru kwa kutupokea vizuri na kwa ukarimu wao unaotufanya tujisikie tuko nyumbani katika huu mji ambao ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu na Chama chetu.
Ndugu Wajumbe;
  Napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kwa matayarisho mazuri ya Mkutano huu wa Nane wa Taifa wa CCM.  Natoa pongezi maalum kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa chini ya uongozi mahiri wa Katibu Mkuu Ndugu Wilson Mukama na Kamati  zote za Maandalizi ya Mkutano kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya ya kuwezesha Mkutano huu kufanyika.  Kwenu nyote nasema hongereni na asanteni sana.
Ndugu Wajumbe;
Karibuni tena Kizota.  Nasikitika kwamba matumaini yangu ya kufanya Mkutano Mkuu katika ukumbi wetu wenyewe hayakutimia.  Hii ni kwa sababu kazi ya matayarisho imechukua muda mrefu kuliko nilivyotazamia.  Tumechelewa kupata kiwanja kilichokidhi mahitaji yetu na matazamio yetu.  Kwanza tulipata kiwanja nyuma ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).  Lakini tukaona ni mbali mno na walipo wananchi.  Tukaja kupata kiwanja kingine juu ya Kilimani Club ambacho hakikuwa kikubwa cha kutosha.  Mapema mwaka huu ndipo tulipopata kiwanja eneo la Makulu  ambacho kinakidhi sifa za kuwa kikubwa cha kutosha na kuwa karibu na katikati ya mji wa Dodoma.  Tumekiafiki  na matayarisho ya kuanza ujenzi yamekamilika.  Leo asubuhi tumeweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa Ukumbi wa Mkutano (Dodoma Convention Centre).  Baadae utafuta ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya CCM na jengo la Hoteli ya Kisasa.
Wageni Karibuni
Ndugu Wajumbe;
Kama mjuavyo Chama cha Mapinduzi kina marafiki wengi Afrika na kwingineko duniani.  Tumekuwa na mazoea ya kualikana katika mikutano mikuu yetu.  Safari hii tumefanya hivyo tena.  Kwa niaba yenu niruhusuni niwashukuru sana wageni wetu wote wa kutoka vyama rafiki Afrika na duniani kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kujumuika nasi siku ya leo. Kuwepo kwao ni kielelezo tosha cha udugu na urafiki uliopo baina ya vyama vyetu na nchi zetu ambao hatuna budi kuudumisha, kuuendeleza na kuukuza.    Hali kadhalika, nawashukuru Mabalozi wa Nchi za Nje na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa walioweza kuja kushiriki nasi katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano wetu.
Ndugu Wajumbe;
Tunawakaribisha kwa furaha na upendo mkubwa viongozi na wawakilishi wa vyama vya siasa vya hapa nchini kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM  siku ya leo.  Tunawashukuru kwa moyo wao wa uungwana kwani tofauti za vyama si uadui.  Wamethibitisha jinsi demokrasia ya vyama vingi inavyozidi kustawi na kukomaa hapa nchini.
Nawashukuru sana pia, viongozi wetu wa dini na wananchi mbalimbali waliojumuika nasi.  Kuwepo kwao ni jambo la faraja kubwa.  Dua za viongozi wa dini zitasaidia kuponya na kuupa baraka mkutano wetu uende salama, uwe wa mafanikio  na kuwafanya wale wote wasiokiombea mema Chama chetu watahayari na kufadhaika.
Karibuni Diaspora
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuwatambua na kuwakaribisha viongozi na wananchama wa Chama chetu waliopo nje, Marekani, Italia, India na Uingereza. Ndugu zetu hawa kwa upenzi wao kwa Chama wamesafiri masafa marefu kuja kushiriki nasi.  Hawa wanastahili pongezi maalum kwa jinsi wanavyopeperusha bendera ya CCM na kueneza sera zake. Naomba tuwape makofi ya nguvu.
Agenda ya Mkutano
Ndugu Wajumbe;
Agenda ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa Nane wa Chama cha Mapinduzi ina mambo makuu manne.  Kwanza kufanya marekebisho ya Katiba ya Chama cha Mapinduzi.  Mengi ya marekebisho hayo yanatokana na uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake cha trehe 11 – 12 Aprili 2011 wa kufanya mageuzi ndani ya Chama.  Miongoni mwa matunda ya mageuzi hayo ni kuundwa kwa Baraza la Ushauri na Wajumbe wa NEC kuchaguliwa Wilayani badala ya Mikoani.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Halmashauri Kuu ya Taifa ina mamlaka ya kufanya marekebisho ya Katiba na marekebisho hayo kutumika.  Hata hivyo, marekebisho hayo hayana budi kuletwa katika Mkutano Mkuu wa Taifa ili yaingizwe rasmi kwenye Katiba.  
Ndugu Wajumbe;
  Jambo la pili litakuwa ni kwa Serikali zetu mbili kutoa taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2010 – 2015 tangu baada ya uchaguzi mkuu hadi sasa.  Vile vile, tutapokea Taarifa ya Halmashauri Kuu ya Chama kuhusu kazi za Chama kwa miaka mitano iliyopita.  Jambo la nne na la mwisho ni kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti, Makamu wake wawili na Wajumbe wa NEC wa Kundi la Zanzibar na Tanzania Bara.
Ndugu Wajumbe;
Tofauti na mikutano iliyopita, Halmashauri Kuu ya Taifa inapendekeza kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wajigawe katika makundi matano kujadili taarifa ya kazi za Chama na zile za utekelezaji wa Ilani.  Kisha kila kikundi kitatoa taarifa ya maoni na mapendekezo yake.  NEC ilifikiria iwe hivyo ili kutoa muda wa kutosha kwa wajumbe kujadili taarifa hizo muhimu katika utaratibu wa zamani wa mtu mmoja kila mkoa kuitwa kusoma, wajumbe hawapati fursa ya kutosha ya kuzijadili taarifa zinazotolewa.
Kuimarisha Chama Kazi Endelevu
Ndugu Wajumbe;
Katika hotuba yangu ya kushukuru baadaya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa Maalum wa tarehe 25 Juni, 20067, pamoja na kuzungumzia mambo mengine, nilisisitiza umuhimu wa kuimarisha Chama chetu.  Nilitoa maoni yangu kwa upana kiasi kuhusu mambo ya kuzingatia.  Leo tena, katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu huu narudia kusisitiza jambo hili.  Nafanya hivyo kwa sababu hilo ndiyo jukumu la kudumu na jukumu la kwanza na la msingi kwa kila kiongozi na kila mwanachamawa CCM.  Isitoshe, kwa hali ilivyo sasa, kuimarisha Chama cha Mapinduzi lazima iwe agenda kuu ya kila mmoja wetu.  Ni ukweli ulio wazi kuwa ustawi na uhai wa Chama unategemea viongozi na wanachama kufanya kazi ya ziada kuimarisha Chama chao.


Ndugu Wajumbe;
Bahati nzuri, chini ya uongozi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Lt. Yusuf Rajab Makamba tarehe 19 Desemba, 2006 ulianzishwa Mradi wa Kuimarisha Chama.  Mradi huo ndiyo uliokuwa dira na mwongozo wetu wa kufanya kazi za Chama tangu wakati huo mpaka leo.  Wajibu wa kila kiongozi na kila mwanachama na kila kikao cha kila ngazi vimeainishwa vizuri.  Pia, uliwekwa utaratibu mzuri wa kufuatilia utekelezaji wake. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa utaratibu maalum uliwekwa wa kutoa tuzo kwa Mikoa iliyofanya vizuri katika utekelezaji wa vipengele mbalimbali vya uimarishaji wa Chama kwa mujibu wa Mradi huo.  
Ndugu Wajumbe;
Kazi ya kuimarisha Chama chetu ni jukumu endelevu kwa kila mwanachama wa CCM, kila kiongozi wa CCM na kila mtumishi wa CCM.  Kwa sababu hiyo, Mradi wa Kuimarisha Chama ni mchakato usiokuwa na ukomo.  Ni kazi ya kudumu na wala siyo tukio lililoanzishwa na Katibu Mkuu Lt. Yusufu Rajabu Makamba na kukoma siku alipostaafu.
Tuongeze Wanachama
Kazi ya kuingiza wanachama wapya ni ya kudumu katika uhai wa Chama cha Mapinduzi.  Hii siyo kazi ya msimu wa uchaguzi wa ndani ya Chama au wakati wa kura za maoni na hivyo kugeuzwa kuwa ni kwa ajili ya kuwapigia debe watu wanaotafuta vyeo.  Lazima wakati wote tuwe tunaingiza wanachama wapya lakini pia lazima tuzingatie utaratibu ulioelekezwa na Katiba ya CCM.  Hatuna budi kuhakikisha kuwa tuna wanachama walio waumini wa kweli na wapenzi wa dhati wa CCM, itikadi yake na sera zake na zile za Serikali zake.
Ndugu Wajumbe;
Wanachama ndiyo nguvu kuu ya uhai na ushindi wa CCM.   Lazima Chama chetu kiwe na Jeshi kubwa la wanachama walio tayari kukijenga, kukisemea na kukipigania.  Kuwa na Wanachama wengi ambao ni waumini wa kweli wa Chama chetu ina maana ya kuwa na kura nyingi za msingi za kuanzia katika uchaguzi wa dola.  Pia wanachama ni nyezo muhimu ya CCM kupata kuungwa mkono na wananchi hasa pale ambapo wanachama wataifanya ipasavyo kazi ya Chama ndani ya umma.  Kila mwanachama akifanya kwa mafanikio kazi ya kushawishi wananchi kupigia kura wagombea wagombea wa CCM tutapata kura nyingi za uhakika.
Tuwe na Viongozi Wazuri
Ndugu Wajumbe;
Kazi ya kuhakikisha kuwa Chama cha Mapinduzi kina viongozi wazuri ni ya kudumu na wala siyo ya msimu wa kuchuja majina ya wagombea.  Lazima Chama chetu kiwe na viongozi ambao ni waumini wa dhati wa itikadi yetu na wanaozijua vyema sera za Chama cha Mapinduzi na Serikali zake.  Wao ndio wanaotarajiwa kuonesha njia kwa kuelimisha wanachama na wananchi.  Viongozi wa CCM lazima wawe hodari wa kufafanua sera na masuala mbalimbali yahusuyo Chama chetu na Serikali zake.  Hawataweza kufanya hivyo kama wao wenyewe ni maamuma.  Kiongozi mzuri wa Chama cha Mapinduzi ni yule ambaye ni jasiri kukitetea Chama cha Mapinduzi na kama hapana budi yuko tayari kujitolea muhanga.  Kuwa na kiongozi ambaye haguswi wala kusikitishwa na hali mbaya ndani ya Chama au hujuma dhidi ya Chama ni sawa na kutokuwa na kiongozi.  Bora asiwepo.  Na kuwa na kiongozi ambaye yeye mwenyewe anafanya vitendo viovu dhidi ya CCM na Serikali zake ni kuwa na nyoka ndani ya nyumba.  Ni jambo hatari lisilokubalika na halistahili kuvumilika.  Tukiwajua tuwaseme, tuwashughulikie, wachague wanapotaka kwenda.  


Ndugu Wajumbe;
Kiongozi mzuri wa CCM lazima awe muaminifu na muadilifu na lazima wanachama na jamii imuone hivyo.  Chama chetu kinashindania kushinda akili na mioyo ya Watanzania na hiyo ndiyo kazi tunayomtarajia kiongozi wetu afanye katika jamii.  Hii ndiyo hasa kazi ya Chama ndani ya umma.  Lakini, ili kiongozi wetu aweze kuifanya kwa mafanikio taswira yake mbele ya jamii ni kitu muhimu.  Awe na taswira nzuri mbele ya wananchi.  Kama jamii inamuona kuwa si mtu muadilifu itakuwa taabu sana kwake kufanikisha jukumu la msingi la Chama chetu.  Hivyo ndugu zangu, lazima tuhakikishe kuwa viongozi wetu wanakuwa waadilifu ili wasigeuke kuwa balaa na hasara kwa Chama.
Ndugu Wajumbe;
Baada ya kukamilisha mchakato wa uchaguzi ngazi ya taifa, tutatengeneza na kutekeleza programu maalum ya kutoa mafunzo kwa viongozi wa Chama kuanzia ngazi ya Tawi hadi Taifa.  Hali kadhalika, tutaendeleza na kukamilisha kazi ya ukarabati na upanuzi wa Chuo cha Ihemi ili kiwe kitovu cha kutoa mafunzo ya siasa kwa makada na viongozi wa Chama na Jumuiya zake kama ilivyokuwa inafanywa katika Chuo cha CCM cha  Kivukoni na vyuo vyake vya kanda.
Ndugu Wajumbe;
Bahati nzuri vyama vya ukombozi vya nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika vimekubaliana kuwa Chuo cha Ihemi kiwe Chuo cha Mafunzo ya siasa kwa makada wa vyama vyao pia.  Ni heshima kubwa kwa CCM, lakini pia inakipa Chama chetu wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa Chuo hicho kinawekwa katika viwango vya kimataifa.  Tuko tayari na tutajipanga ipasavyo kutimiza wajibu wetu huo wa kihistoria.
Vikao Vifanyike Ipasavyo
Ndugu Wajumbe;
Ni kazi endelevu kwetu sote, wanachama na viongozi, kuhakikisha kuwa vikao vinafanyika kwa wakati na kwamba mikutano inaendeshwa vizuri na ina agenda zenye maslahi ya kujenga Chama na kuendesha nchi.  Pia, ni muhimu kuhakikisha kuwa kinachoamuliwa kinatekelezwa ipasavyo.  Naamini kwamba mafunzo tutakayotoa kwa viongozi na watendaji wa Chama kuhusu wajibu wao na jinsi ya kuutekeleza yatasaidia sana kuimarisha CCM.
Watendaji Mahiri
Ndugu Wajumbe;
Kwa Chama chetu kuwa na watendaji wazuri ni jambo lisilokuwa na mjadala.  Lazima tuwe na watendaji ambao ni makada wazuri na watu mahiri kwa kazi zao.  Wawe ni watu ambao wana uelewa mzuri wa sera za Chama na kwamba wanaweza kuzifafanua, kuzieneza na kuzitetea.  Pia, wawe ni watu wanaojua vyema kazi yao ya utendaji, kwa mujibu wa shughuli zao wanazozifanya.  Ni vyema kwa kazi za kitaalamu tukapata watu wataalamu wa kazi hizo.  Ni muhimu sana tukayazingatia haya kwani utendaji mzuri katika Chama ni nguvu muhimu sana ya kukifanya Chama chetu kuwa imara.  Chama chetu kiwe na mipango thabiti ya kuwaendeleza watumishi wake na kama hapana budi kuwadhamini wakasome. Tufanye hivyo.
Bila ya shaka mtakumbuka kuwa tarehe 3 Novemba, 2007, pale Kizota, niliahidi kuwa tutaboresha maslahi ya watumishi wa Chama.  Tumetimiza ahadi hiyo.  Leo nasema kuwa tutajitahidi kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi wetu kadri uwezo utakavyoruhusu.
Tujitegemee
Ndugu Wajumbe;
Lazima Chama chetu kiwe na uwezo wake chenyewe wa kujisimamia na kujiendesha.  Kiwe na fedha za kutosha na vitendea kazi.  Hivi sasa hatuko hivyo.  Hatuna budi kuongeza maarifa na juhudi za kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kujitegemea kifedha bila ya kujali kama kuna ruzuku au hakuna.  Jambo hili sasa liwe ni la kufa na kupona kwetu kuhakikisha linakuwa. Iwe agenda kuu ya Chama katika ngazi zote.  Kila mmoja afikirie nini cha kufanya na kifanywe.  Jambo la kuzingatia ni kufanya shughuli halali.  Fursa zipo tuzitumie.  Tusikubali kushindwa kwenye azma kwani hiyo itakuwa maangamizi wa CCM.  Lazima tushinde.
Ndugu Wajumbe;
Mtakumbuka pia kwamba niliahidi kuimarisha usafiri ndani ya Chama.  Ahadi hiyo tumeitimiza.  Kila Mkoa na kila Wilaya imepata gari mpya tena gari nzuri na imara.  Gari hizi tukizitunza vizuri zitatuwezesha katika  uchaguzi ujao bila ya taabu.  Kwa Mikoa na Wilaya mpya mipango ya kuwapatia magari iko mbioni. Kila Jumuiya tuliipatia magari yasiyopungua matatu.
Jumuiya za Chama
Ni wajibu wa kudumu wa Chama chetu kuhakikisha kuwa Jumuiya zake zinaimarika na kutimiza ipasavyo wajibu wake.  Jumuiya ndiyo mkono mrefu wa Chama cha Mapinduzi kuufikia umma mpana wa Watanzania hasa wale ambao si wanachama.  Jukumu letu ni kuhakikisha kuwa watu hao wanakuwa wanachama au wapenzi na marafiki wa CCM.  Kwa hiyo, kuwepo kwa Jumuiya ni fursa nzuri kwa Chama cha Mapinduzi kuungwa mkono na watu wengi ili wakati wa uchaguzi tuweze kupigiwa kura na kupata ushindi.  Jumuiya lazima zihakikishe kuwa zinatimiza ipasavyo wajibu wake ili wasiipotezee CCM fursa hii adhimu.
Ndugu Wajumbe;
  Kwa muhtasari, hayo ndiyo baadhi ya mambo ya msingi ya mradi wa kuimarisha Chama.  Mtakubaliana nami kuwa haya yote ndiyo kazi na wajibu wa kila mmoja kufanya.  Ni kazi endelevu isiyokuwa na ukomo.  Tupo kwa ajili hiyo na rai yangu kwenu ni kuhakikisha kuwa kila mwanachama na kila kiongozi anatimiza ipasavyo wajibu wake.
Mageuzi Ndani ya Chama
 Ndugu Wajumbe;
Kwa dhamira ya kuendelea kukiimarisha zaidi, Chama cha Mapinduzi, katika mkutano wake wa tarehe 11-12 April, 2011, Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua kuanzisha mchakato na kufanya mageuzi ndani ya Chama.  Lengo kuu la uamuzi huo ni kukiwezesha Chama chetu kuwa na taswira inayovutia katika mitazamo na hisia za wanachama wake na wananchi.
Kimsingi NEC inataka tukiwezeshe Chama cha Mapinduzi kiendelee kupendwa na kuaminiwa na wananchi wote wa Tanzania.  Tunataka wanawake na wanaume, wadogo na wakubwa, maskini na matajiri, wanyonge na wenye nguvu waone kuwa CCM ndiyo kimbilio lao.
Ndugu Wajumbe;
 Kwa ajili hiyo mageuzi ya ndani ya Chama yamejengeka juu ya misingi ifuatayo:-
Kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kuwa na makada na viongozi mahiri, waadilifu na waaminifu kwa Chama chao;
Kukiwezesha Chama kuwa na sera zinazojali maslahi ya wengi na kusukuma mbele kwa kasi maendeleo ya taifa letu;
Kukiwezesha Chama kuwa na muundo na mfumo wa uendeshaji ulio nyumbulifu na unaokifanya kuwa karibu na wanachama na wananchi;
Kukiwezesha Chama kujitegemea kimapato na kiuchumi ili kiweze kuendesha shughuli zake kwa uhakika, uhuru na heshima;
Kukiwezesha Chama kuwa na watu hodari wa kazi na Makada wazuri ambao wanalipwa vizuri na kuwezeshwa kutekeleza majukumu yao;
Kukiwezesha Chama kuwasiliana na umma kwa urahisi na kupambana na propaganda chafu za vyama vya siasa; na
Kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kupambana na maovu ndani ya Chama na katika jamii likiwemo tatizo la rushwa na mengineyo.

Ndugu Wajumbe;
Katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa iliamuliwa kuwa kutokana na umuhimu wa hoja na haja ya kufanya mageuzi ndani ya Chama utekelezaji wa mageuzi uanze mara moja.  Aidha, pawepo na progamu ya utekelezaji unayoainisha nini kinafanyika lini na mhusika ni nani!  Bila ya shaka mtakumbuka kuwa katika kikao kile, tuliunda upya Kamati Kuu na kuteua Sekretarieti mpya.  Vile vile iliamuliwa kuwa tufanye marekebisho katika muundo wa Chama na moja ya  matokeo yake ni Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kuchaguliwa kutoka wilayani.  Nafasi za NEC za mikoa zikafutwa na zile za taifa zikapunguzwa.  Aidha, limeundwa Baraza la Taifa la Ushauri ambalo wajumbe wake ni viongozi wakuu wa Chama wastaafu.  Wanapata fursa ya kukaa na kutoa ushauri kwa Chama na viongozi wake.
Ndugu Wajumbe;
Tuliamua, pia, kuunganisha chaguzi za Chama na Jumuiya zifanyike mwaka mmoja.  Shabaha ya uamuzi huo ni kutaka kujipa muda wa kutosha wa kujenga Chama na Jumuiya zake na kujiandaa kwa chaguzi za dola.  Uamuzi huo umeokoa takriban mwaka mzima ambao tulikuwa tunautumia kwa uchaguzi.  Vile vile Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua kwamba mgao wa fedha unatokana na mapato Chama zinazopelekwa kwenye Matawi na Mashina uongezwe.  Lengo ni kuziwezesha ngazi hizi muhimu za Chama kufanya kazi vizuri zaidi.


Ndugu Wajumbe;
Suala la nidhamu na maadili ya viongozi na wanachama lilisisitizwa sana kwa sababu ya umuhimu wake kwa taswira ya Chama chetu mbele ya jamii na wanachama wake.  Pia, kutokana na ukweli kwamba ni kilio cha wanachama na wananchi cha kutaka tuiondowe taswira mbaya dhidi ya Chama iliyopo katika jamii kuwa ni Chama kisichokerwa na rushwa.  Hicho ni kilio cha dhati kwa watu wenye nia njema na CCM:  Chama chao, wanachokipenda na kukiamini.  Chama ambacho bado hakina badala yake wa kuiongoza vyema nchi yetu na watu wake.
Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua mambo mawili yafanyike.  La kwanza, mfumo mzima wa kushughulikia masuala ya usalama na maadili katika Chama utazamwe upya na uimarishwe.  Pili, Chama kichukue hatua na lazima kionekane kinachukua hatua dhidi ya viongozi na wanachama wasiokuwa waadilifu na waaminifu wanaofanya sura ya Chama ichafuke mbele ya jamii.  NEC iliagiza wenyewe wajipime na kuamua na wasipofanya hivyo vikao husika katika Chama vichukue hatua.
Ndugu Wajumbe;
Hayo ni baadhi tu ya mambo muhimu yaliyoamuliwa yafanyike katika kufanya Mageuzi Ndani ya Chama.  Utekelezaji wake umeanza.  Yapo yaliyokamilika na yapo yanayoendelea kutekelezwa.  Yapo mambo mengi ambayo ni endelevu kama vile mapambano dhidi ya rushwa.  Hatuna budi kuendelea kulikemea na kusimama kidete kupambana na tatizo hili mpaka likomeshwe.  Ni kwa maslahi na heshima ya Chama chetu kuendesha mapambano haya bila ya woga mpaka tushinde.  Tukishindwa itakuwa hatari kwa uhai wa Chama chetu.
Umoja ni Ushindi
Ndugu Wajumbe;
Mara ya mwisho tulipokutana tarehe 11 Julai, 2010, tulikuwa tunajipanga kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.  Mliniteua mimi na Dkt. Mohamed Ghalib Billal kupeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Pia tulipitisha Ilani ya Uchaguzi ya 2010-2015.  Siku moja kabla ya Mkutano Mkuu, Halmashari Kuu ya Taifa ilikuwa imemteua Dkt. Ali Mohamed Shein kupeperusha bendera yetu kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar.
Bahati nzuri tumepata ushindi kwa nafasi zote hizo za juu za uongozi wa taifa letu.  Pia tulifanikiwa kupata Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wengi zaidi kuliko vyama vya upinzani.  Kwa sababu hiyo, tumeunda Serikali zote mbili za nchi yetu na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi unaendelea vizuri.
Ndugu Wajumbe;
Kwa upande wa Zanzibar, tuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa na mambo yanakwenda vizuri.  Tuzidi kuunga mkono na kuwatakia heri Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd.  Tunawapongeza sana kwa mafanikio yaliyopatikana.  Zanzibar ina amani na umoja unaozidi kuimarika.  Tunatakiwa tuendelee kuiunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili ifanikiwe zaidi.
Ndugu Wajumbe;
Uchaguzi uliopita kwa upande wa Tanzania Bara ulikuwa na changamoto nyingi ambazo hatukuzizoea wala kujiandaa nazo.  Zinaelezea matokeo tuliyoyapata jambo ambalo linatulazimu kuwa makini zaidi katika uchaguzi ujao.  Tusikubali kushtukizwa tena.  Lakini, jambo moja lililo dhahiri ni kwamba umoja na mshikamano miongoni mwa wana-CCM ndiyo uliotuwezesha kukabili changamoto hizo na kupata ushindi tulioupata.  Bila ya hivyo, mbinu hasi zilizotumika zingetufanya tushindwe.
Napenda ukweli huu uwepo katika vichwa na mioyo ya wana-CCM na sisi viongozi wao tuliochaguliwa hivi majuzi na watakaochaguliwa katika Mkutano huu.  Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema: Umoja ni Nguvu, ni kweli kabisa na sisi ni mashahidi.  Nami napenda kuongeza kwa kusema kuwa Umoja ni Ushindi.
Ndugu Wajumbe;
Nawaomba wakati wote wa mkutano na baada ya mkutano tukumbuke na kuzingatia Umoja.  Tuishikilie kamba ya Umoja isituponyoke.  Tuimbe Umoja kimoyo moyo na tubainishe wazi wazi kwa kauli na matendo yetu kuwa: Umoja ni Nguvu Utengano ni Udhaifu! Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!.  Napenda kuona kuwa tunatoka hapa tukiwa kitu kimoja, tukiwa watu tunaopendana na tulioshikamana.   Nataka tuondoke katika Mkutano sote tukivuta kamba upande mmoja badala ya kuvutana.  Nataka tuazimie kukabiliana na kauli, matendo au watu wanaopandikiza chuki na kuhatarisha umoja ndani ya Chama chetu na miongoni mwetu.    Nataka kaulimbiu ya ujumbe wa Mkutano huu uwe Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!   Tukiendelea kuwa watu tunaovutana na kuhasimiana hatutaweza kukijenga Chama chetu wala kuwatafutia ushindi wagombea wa Chama chetu.  Tutakuwa sawa na ule msemo wa Kiswahili usemao: “vita vya panzi furaha ya kunguru”  Tusijigeuze panzi na wala tusikifikishe Chama chetu kiwe hivyo.
Ndugu Wajumbe;
Mtakubaliana nami kuwa harakati za kutafuta uongozi ndani ya Chama au uteuzi wa kugombea katika chaguzi za dola imekuwa ndiyo chanzo kikuu kinacholeta mifarakano na kuvuruga umoja ndani ya Chama chetu.  Hili ndugu zangu siyo sawa hata kidogo.  Kugombea uongozi ni haki ya msingi ya mwanachama na raia wa Tanzania.  Kwa nini mtu achukiwe au aonekane adui kwa kuamua kuitumia haki yake hiyo?  Kwa nini afanyiwe vitimbi, vitendo viovu au njama za kuhujumiwa?  Nani mwenye haki zaidi ya mwanachama ama raia mwenzake?  Ni ubabe na jeuri ya pesa isiyokuwa na msingi.  Ni ubinafsi na uchu wa madaraka uliopitiliza mipaka.  Watu wa namna hiyo ni hatari sana kwani wanaweza hata kuua au kukivuruga Chama chetu kizuri kama tamaa zao zisipokidhiwa.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wale wote wanaochukiana kwa sababu ya kugombea watakafakari upya misimamo yao.  Wafanyayo siyo sahihi, wanaathiri nguvu na uhai wa Chama chetu.  Naomba Kamati za Siasa za ngazi zote ziwatambue watu hao na kuwaita kuwapatanisha.  Naomba wahusika watoe ushirikiano wao.  Hata wale wanaohisi kuwa hawakutendewa haki katika uchaguzi, walidhulimiwa au hata kushindwa kwa sababu ya vitendo vya rushwa, wakumbuke kuwa Chama chetu kina utaratibu wa kushughulikia malalamiko yao.  Wautumie utaratibu huo badala ya kufanya vitendo vinavyokigawa na kukivuruga Chama chetu.  Kulalamika katika vyombo vya habari, kufanya ghasia au kuchochea migawanyiko hakutaleta ufumbuzi.
Ndugu Wajumbe;
Niruhusuni nitumie nafasi hii kuwasihi wale wote wenye tamaa ya kugombea uteuzi ndani ya Chama wasituulie Chama chetu.  Kuwa na tamaa ya kugombea Urais, Ubunge na Udiwani si kosa ni haki ya mwanachama na ni haki ya raia wa nchi hii.  Jambo ambalo halikubaliki na gumu kulivumilia ni kufanya vitendo vya kuwagawa wanachama na Chama chetu.  Kuwalazimisha au kuwashinikiza kujiunga na kundi fulani siyo sawa.  Kumchukia mtu kwa sababu naye anagombea au amekataa kukuunga mkono au kumuunga mkono umpendae ni jambo baya.  Unaifanya demokrasia iwe haina maana au kichekesho.  Na, lililo baya kupita kiasi ni kutumia fedha kushawishi, kuwarubuni au kuwanunua watu kukuunga mkono au kumuunga mkono mgombea wako au kujiunga na makundi.  Hili ni jambo haramu na ni utovu wa maadili usiokubalika ambao lazima tuukatae, tuukemee na tuupige vita kwa nguvu zetu zote.  Naomba wote tushirikiane katika mapambano haya kwa heshima ya Chama chetu.
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
Ndugu Wajumbe;
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 unakwenda vizuri kwa Serikali zetu zote mbili.  Taarifa zitakazotolewa na Waziri Mku, Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa upande wa Serikali ya Muungano na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zitathibitisha ukweli huu.  Niruhusuni nichukue muda wenu kidogo nizungumzie baadhi ya mambo yahusuyo shughuli za Serikali.
Nchi Iko Salama
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuanza kwa kuwahakikishia kuwa Tanzania iko salama pamoja na kuwepo matukio ya hapa na pale.  Mipaka yetu iko salama.  Hakuna tishio lo lote la kiusalama la kutufanya tuhamanike.  Hata mpaka wetu na Malawi uko salama pamoja na kuwepo kwa maneno maneno yahusuyo nchi zetu mbili kutofautiana wapi ulipo mpaka halali.  Hakuna jambo lo lote linalofanywa upande wa wenzetu ambalo linatufanya tuwe na mashaka ya usalama wa nchi yetu kuwa hatarini.  Kwa sababu hiyo hatujaiona haja ya kusogeza Majeshi yetu mpakani na anayesema tumefanya hivyo ni muongo.  Apuuzwe na kushushuliwa.
Ndugu Wajumbe;
Tumeendelea na juhudi za kuimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kuwajengea uwezo, zana na vifaa vya kisasa vya kivita.  Lengo letu ni kukuza nguvu ya kimapigano ya Jeshi letu na kuimarisha utayari wake kivita.  Hali kadhalika, tumeendelea kuboresha maslahi ya wanajeshi na mazingira yao ya kufanyia kazi na ya kuishi. Kwa upande wa usalama wa raia, yaani maisha na mali zao, matukio ya uhalifu yanaendelea kupungua.  Hali hii inaashiria kuwa Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri.  Kama tufanyavyo kwa JWTZ, tutaendeleza juhudi za kuimarisha Jeshi la Polisi kwa watu, zana na vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi.  Tutaendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kufanyia kazi na ya kuishi ya Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama.
Ndugu Wajumbe;
Pamoja na kutokuwepo kwa tishio lililo dhahiri la shambulio la kigaidi, wakati wote  vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko katika hali ya tahadhari kuepuka kushtukizwa.  Kama mnavyokumbuka mwaka 1998 Ubalozi wa Marekani hapa nchini ulishambuliwa na ndugu zetu 11 walipoteza maisha.  Hivyo basi, kuchukua tahadhari ni jambo la busara kufanya.  Aidha, tuko katika hali ya tahadhari dhidi ya uharamia wa kuteka meli katika Bahari Kuu ya Hindi.  Takriban mwaka mzima umepita bila ya matukio ya kutekwa nyara meli katika bahari yetu .  Hata hivyo hatuachi kuchukua tahadhari.
Ndugu Wajumbe;
Matukio ya hivi karibuni ya vurugu zenye mwelekeo wa  kidini yanasikitisha na kusononesha.  Ni mambo ambayo hayafanani na sifa ya nchi yetu ya kuheshimiana na kuvumiliana  pamoja na kuwepo tofauti  zetu za dini, kabila rangi au maeneo tutokako. Vitendo hivyo havikubaliki na Serikali haitawavumilia au kuwaonea muhali wale wote wanaohusika na kuchochea vurugu hizo.  Tumechukua hatua na tutaendelea kuchukua hatua bila ya ajizi.  Ombi langu na wito wangu kwa viongozi na wafuasi wa dini nchini kuhubiri dini zao huku wakitambua na kuzingatia umuhimu wa kuheshimu imani za wengine na kuvumiliana.  Tusipofanya hivyo nchi yetu tutaingiza kwenye matatizo yasiyostahili  kuwepo.
Ndugu Wajumbe;
Inatia moyo kuona kuwa watu wenye nia njema na nchi yao ni wengi.  Kwa sababu hiyo pamoja na jitihada za baadhi ya watu wasiyoitakia mema nchi yetu hawajafanikiwa kuwagawa na kuwafarakanisha Watanzania.  Nawaomba Watanzania wenzangu tuwe na moyo huo huo na sisi katika Serikali tutaendelea kumchukulia hatua mtu ye yote anayetaka kutuvurugia amani na utulivu wa nchi yetu na watu wake.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali haitamuonea mtu ye yote asiyehusika.  Tutaendelea kuidumisha sifa yetu ya kuendeleza utawala bora, kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia utawala wa sheria.  Kadhalika tutaendelea kuheshimu mgawano wa madaraka miongoni mwa mihimili mikuu ya dola.  Nafurahi kwamba mpaka sasa mambo yanakwenda vizuri.
Muungano Imara
Ndugu Wajumbe;
Muungano wetu ni imara pamoja na kuwepo vitendo vyenye lengo la kuudhoofisha vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa siasa na wa dini hasa kule Zanzibar.  Jambo linalosikitisha ni watu hao kutumia njia za vitisho na ghasia ili kuwalazimisha watu kuwaunga mkono.  Njia hizo hazikubaliki na wala hazitavumiliwa.
Inastaajabisha mambo hayo kufanyika hivi sasa wakati kuna Tume ya Katiba.  Kama mtu ana maoni yo yote kuhusu Muungano ayafikishe tu, yatapokelewa na kupimwa.  Vile vile Kamati ya Pamoja ya Serikali zote mbili inayowakutanisha Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano imekuwa inafanya kazi nzuri kutatua kero za Muungano.  Kama mtu analo jambo analotaka lipatiwe jawabu awasilishe kwa wahusika litashughulikiwa.  

Hali ya Uchumi
Ndugu Wajumbe;
Katika Mkutano Mkuu Maalum wa Julai, 2010 hapa Kizota, nilielezea mafanikio tuliyoyapata na changamoto tulizokumbana nazo katika kukuza uchumi wa nchi yetu na kupunguza umasikini. Nilieleza pia nia yetu ya kuendelea kupambana na changamoto zilizokuwa mbele yetu pamoja na ugumu unaotokana na hali ya kuyumba kwa uchumi wa dunia ambamo na sisi pia tumo.  Kwa ajili hiyo mwaka 2011 tulizindua Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano(2011/12 – 2015/16).
Mpango huu ni wa kwanza kati ya mitatu katika safari yetu ya kutekeleza Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025.  Kwa mujibu wa Dira yetu hiyo, tunatarajia ifikapo mwaka 2025 nchi yetu itaondoka katika kundi la nchi maskini sana duniani na kuwa nchi ya uchumi wa kati.  Yaani tunataka pato la wastani la Watanzania litoke kwenye dola za Kimarekani 545 za sasa hadi kufikia dola za Kimarekani 3,000.  Lengo hilo ni kubwa linalohitaji mipango thabiti na uwekezaji makini wa Serikali na sekta binafsi.  Pia inahitaji kuwepo kwa nidhamu ya dhati ya viongozi na wananchi wa Tanzania.
Ndugu Wajumbe;
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo umekwishaanza.  Lengo la jumla katika Mpango wa kwanza ni Kufungulia fursa kwa ukuaji wa uchumi; wa pili ni Ujenzi wa mazingira ya maendeleo ya viwanda;  na wa tatu ni Kuimarisha ubunifu na ushindani kimataifa.  Tayari miradi ya kimkakati imekwishaainishwa na inapewa kipaumbele katika bajeti ya Serikali na ubia baina ya sekta binafsi na sekta ya umma. Katika kila hatua suala la kukuza ajira limepewa umuhimu mkubwa kwani lengo letu ni kuwa na ukuaji wa uchumi unaojumuisha maisha ya watu.  Vijana ni walengwa wakubwa.
 Mwelekeo wa uchumi wetu ni mzuri.  Kasi ya ukuaji wa uchumi iliyokuwa asilimia 6.4 mwaka wa jana inatarajiwa kufikia asilimia 7 mwaka huu.  Mauzo yetu ya nje yanazidi kukua na kuongezeka.  Kwa mfano mwaka 2005 ilikuwa dola za Kimarekani milioni 2,945.5 na sasa ni milioni 7,461.2.  Akiba yetu ya fedha ya kigeni nayo ni nzuri.  Hivi sasa ni dola za Kimarekani bilioni 4.1 inatuwezesha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi 3.8.
Ndugu Wajumbe;
Changamoto kubwa katika uchumi ni mfumuko wa bei.  Ni kweli umepungua kutoka asilimia 19.8 Desemba, 2011 hadi asilimia 13.5 Septemba, 2012, hata hivyo kupungua huko ni kidogo mno.  Tunaendelea kuchukua hatua za kudhibiti na kupunguza zaidi mfumuko wa bei.  Kwa vile moja ya sababu ni kupanda kwa bei za mafuta. Tumeipa dhamana EWURA kusimamia kwa karibu uagizaji na upangaji wa bei ya mafuta.
  Kwa kuwa bei za vyakula hasa mchele na sukari navyo huchangia kupanda kwa mfumuko wa bei na kuongeza gharama ya maisha mamlaka husika zimeagizwa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanawezeshwa kuagiza bidhaa hizo kwa wingi kutoka kwa nje kwa kuwapatia nafuu ya baadhi ya kodi.  Pamoja na hayo jawabu la kudumu lipo katika kuendeleza mageuzi ya kilimo ili nchi yetu ijitosheleze kwa chakula na kupata ziada kubwa ya kuuza nje.  Hayo ndiyo malengo na hatua zinazochukuliwa katika ASDP, Kilimo Kwanza na SAGCOT.  Ndiyo maana tutaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima, kuimarisha masoko na miundombinu vijijini.
Mapato na Matumizi ya Serikali
Ndugu Wajumbe,
Tunazidi kupata mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.  Makusanyo ya mapato ya kodi Mwezi Agosti 2012, kwa mfano, yalifikia shilingi bilioni 554.8 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi bilioni 147 mwezi Desemba 2005. Mafanikio haya yametokana na juhudi za dhati za Serikali katika kusimamia mabadiliko ya sera na kuimarisha mifumo na taasisi za ukusanyaji wa mapato ya kodi na mengineyo.
Kwa sababu ya kuongezeka huko kwa mapato, bajeti ya Serikali nayo imeongezeka kutoka shilingi trilioni 4.13 mwaka 2005/06 hadi shilingi trilioni 15.12 mwaka huu.  Jambo linaloleta faraja ni kuwa mchango wa Serikali kutokana na bajeti hiyo nao umeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.1 mwaka 2005 hadi trilioni 8.8 mwaka huu.  Utegemezi wa wahisani nao unaendelea kupungua kutoka asilimia 44 mwaka 2005/6 hadi 21.
Ndugu Wajumbe;
Sambamba na kuongeza mapato, nidhamu, udhibiti wa matumizi ya fedha na mali za umma vinazidi kuimarika.  Hii ni kutokana na kuimarika kwa mifumo na kada ya uhasibu katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.  Pia ni matokeo ya kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma.  Hati Chafu katika idara za Serikali zinaendelea kupungua katika taarifa ya ukaguzi kila mwaka.  Hivi sasa tunaelekeza nguvu zetu katika kuhakiki thamani ya fedha zilizotumika na kazi iliyofanyika au huduma iliyotolewa.
Uwekezaji
Ndugu Wajumbe,
Serikali imechukua hatua kadhaa kuboresha mazingira ya uwekezaji na ya kufanya biashara hapa nchini.  Lengo letu ni kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuongeza vitega uchumi nchini na kupanua biashara ndani ya nchi na kati ya nchi yetu na nchi nyingine duniani.  Tunafanya hayo kwa kutambua ukweli kwamba uchumi unakua na kuongezeka pale ambapo uwekezaji unaongezeka.  Takwimu zinaonyesha kwamba uwekezaji umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka katika sekta ya utalii, viwanda, kilimo, madini, fedha,  ujenzi na sasa kwenye utafutaji wa gesi na mafuta.  Tumepata mafanikio makubwa katika utafutaji wa gesi na nchi yetu itakuwa moja ya mzalishaji mkubwa wa gesi.  Mwaka 2011, kwa mfano, kulikuwa na jumla ya miradi 826 yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 7,177 itakayozalisha ajira ya watu 79,000.  Haya ni mafanikio madogo lakini tunaweza kufanya vizuri zaidi.
Tutaendelea kutumia fursa ya kijiografia ya nchi yetu kuvutia uwekezaji na kuifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati.  Ili kufanikisha hayo, tutaendelea kuboresha miundombinu ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na teknohama.
Miundombinu
Ndugu wajumbe;
Moja ya vipaumbele vya juu vya Serikali ya CCM ninayoiongoza ni kuboresha miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na angani nchini. Tumethibitisha hayo kwa mgao wa fedha za bajeti ya Serikali ambapo miundombinu ni ya pili baada ya elimu.  Mwaka huu ni shilingi trilioni 2.4, ambayo ni asilimia 16 ya bajeti ya Serikali ukilinganisha na elimu yenye trilioni 3.6 ambayo ni sawa na asilimia 2.4, na afya yenye shilingi trilioni 1.5 sawa na asilimia 10 ya bajeti ya Serikali. Tunafanya hivyo kwa kutambua mchango muhimu wa sekta ya usafiri kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Usafiri unapokuwa bora na wa uhakika, gharama za usafirishaji zinapungua, shughuli za uzalishaji viwandani na kilimo zinaimarika.  Ni kichocheo kikubwa cha kuibuka kwa fursa mbalimbali za uchumi na kuongeza kasi ya maendeleo na kukuza kipato cha Watanzania waliopo mijini na vijijini.
Ndugu Wajumbe;
Tunafanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa barabara kuliko wakati mwingine wo wote katika historia ya nchi yetu.  Hivi sasa  barabara zenye urefu wa kilometa 11,154 zinajengwa kwa kiwango cha lami katika sehemu mbalimbali nchini.  Tulijipa lengo la kuunganisha mikoa yote  kwa barabara za lami na barabara zote kuu ziwe za lami.
Nafurahi kusema kuwa utekelezaji wake unakwenda vizuri.  Tumeanza kufanikiwa kuifikia ile mikoa ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haifikiki kwa urahisi kwa kukosa barabara za lami.  Katika hotuba yangu ya tarehe 25 Juni, 2006 niliwaambia Wajumbe wa Mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Mtwara, Kigoma na Tabora kuwa kilio chao tumekisikia.  Niliahidi kuwa ujenzi wa barabara katika Mikoa hiyo tutaipa kipaumbele.  Tumetimiza ahadi hiyo na kazi inaendelea kwa kasi na hata wenyewe ni mashahidi.  Karibu tunafikia ndoto yetu ya kwamba hakuna mkoa utakaoachwa nyuma.
Ndugu Wajumbe;
Inafurahisha zaidi  kuona kuwa zaidi ya asilimia 60 ya gharama za ujenzi wa barabara tunazojenga nchini ni fedha zetu wenyewe.   Aidha, uwezo wa  Mfuko wa Barabara (Road Fund) nao umeongezeka sana kutoka shilingi bilioni 58 mwaka 2005 hadi shillingi bilioni 430. Hali hiyo imeongeza uwezo wetu wa kujenga na kukarabati barabara mbalimbali nchini.  Kwa ajili hiyo tumeongeza bajeti ya barabara kwenye Halmashauri zote nchini.
Ndugu Wajumbe;
Pamoja na barabara, tunaendelea kuimarisha viwanja vya ndege, bandari na usafiri wa reli.   Changamoto mbalimbali zinajitokeza katika utekelezaji wa lengo letu na kubwa zaidi ikiwa ni ile ya gharama za ujenzi na ukarabati wa miundombinu kuwa kubwa mno ikilinganishwa na uwezo wetu.  Tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuzikabili changamoto hizo hatua kwa hatua na tunazipunguza.
Elimu
Ndugu wajumbe;
Tumefanikiwa kupanua sana fursa za kuwapatia elimu vijana wetu katika ngazi zote. Kuna watoto wengi katika elimu ya awali, na kwa  elimu ya msingi asilimia 97 ya watoto wenye umri wa kwenda shule wamejiandikisha. Kwa kiwango hicho, tuko mahali pazuri kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2015 kama ilvyoagiwa katika Malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa. Kuhusu elimu ya Sekondari, wananchi na wadau wengine wameitikia wito wa Serikali wa kila Kata kuwa na shule ya sekondari. Kwa sababu hiyo idadi ya shule 3,165 zimejengwa kati ya 2005 na hivi sasa na idadi ya wanafunzi katika shule za sekondari imeongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,884,272 mwaka huu.
Tumepanua sana mafunzo ya ufundi na elimu ya juu.  Hivi sasa nchi yetu ina vyuo vikuu 27 na wanafunzi waliopo vyuoni humo ni zaidi ya 166,484 ikilinganishwa na 40,719 wa mwaka 2005.  Ili kutoa fursa sawa kwa wanafunzi wote tumeongeza sana uwezo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili  iwape wanafunzi wengi mikopo ya elimu.  Bajeti ya Bodi hiyo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 56.1 mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 306.0 mwaka huu.  Wanafunzi wanaopata mikopo wapo 93,176 ukilinganisha na 16,345 mwaka 2005.  Tutaendelea kuongeza fedha ili tuwafikie wanafunzi wengi kadri inavyowezekana.
Ndugu Wajumbe;
Upanuzi mkubwa wa elimu katika ngazi zote nchini umezua  changamoto mbalimbali  kuhusu ubora wa elimu.  Tunazitambua changamoto hizo kuwa ni pamoja na zile za upungufu wa walimu, hususan wa sayansi; upungufu wa vifaa vya maabara, vitabu na nyumba za walimu hasa kwenye maeneo ya vijijini.   Tumejipanga vyema kuzitafutia ufumbuzi na tumeanza kufanya hivyo.  Tumeongeza vyuo vinavyotoa mafunzo ya ualimu ili kuongeza idadi ya waalimu.  Bajeti ya elimu ni kubwa kuliko zote ili kusaidia kutatua tatizo la upungufu wa vitabu, maabara, vifaa vya kufundishia na nyumba za walimu na mahitaji mengineyo.  Hivi karibuni nilipokuwa Mkoani Singida nimewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kuhakikisha kuwa shule zote za sekondari katika maeneo yao zinakuwa na maabara ya sayansi katika miaka miwili ijayo.
Afya
Ndugu wajumbe;
Suala la afya ya Watanzania tunalipa umuhimu mkubwa sana. Tumeongeza bajeti ya afya kutoka shilingi bilioni 271 mwaka 2005 hadi shilingi trilioni 1.5 mwaka huu.  Nyongeza hii ndiyo iliyotuwezesha kutekeleza Sera mpya ya Afya (2007) na Mpango wa Miaka Kumi wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) wa kuitekeleza vyema Sera hiyo. Lengo kuu la sera na MMAM ni kuwapatia Watanzania huduma ya afya iliyo bora katika umbali usiozidi kilometa tano. Vile vile, ni kuimarisha huduma zinazotolewa katika hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katika mpango huu pia tumeazimia kukabili tatizo la upungufu wa madaktari, wauguzi na wataalamu wengi.  Tunaendelea kupanua mafunzo ya wataalamu hao katika vyuo vyetu hapa nchini na hata nje ya nchi.  Tumejenga na tutaendelea kujenga vyuo vipya, wakati huo huo tukipanua vilivyopo.  Tumeendelea kujenga uwezo wa kupambana na maradhi makubwa yanayoua watu wengi.  Tumeelekeza nguvu zetu kwenye maradhi yanayoambukiza kama vile malaria, UKIMWI na kifua kikuu  na yale yasiyoambukiza kama vile saratani, moyo, shinikizo la damu na vifo vya kina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Ndugu Wajumbe;
Kwa maradhi yote mafanikio ya dhahiri yanaendelea kupatikana.  Maambukizi ya virusi vya UKIMWI yanapungua kutoka asilimia 8 hadi asilimia 5.7, vifo kutokana na malaria vimepungua kwa asilimia 40 kwa Tanzania Bara na kwa Zanzibar tunakaribia kutangaza kufutika kwa maradhi hayo.  Tumepanua uwezo wa kutibu maradhi ya moyo ikiwa ni pamoja na kufanya upasuaji wa moyo.  Tumepanua uwezo wa kuchunguza na kutibu maradhi ya kansa.  Tunaendelea kujenga uwezo wa ndani kwa maradhi tunayopeleka wagonjwa wengi nje na mafanikio yanaaza kuonekana.  Safari ni hatua, naamini tutafika kwani mwelekeo wetu ni mzuri.
Umeme na Maji
Ndugu wajumbe;
Tunaendelea kupanua uwezo wetu wa kuzalisha na kusambaza umeme nchini.  Tumeanza safari ya uhakika ya kupunguza kutegemea mno umeme wa nguvu ya maji.  Tunapanua umeme utokanao na vyanzo vingine hasa gesi asilia na makaa ya mawe.  Mipango ya kutumia upepo na mionzi ya jua nayo iko mbioni.  Pamoja na hayo tunayo mikakati ya kupunguza umeme unaozalishwa kwa kutumia mafuta kwa kubadili mitambo hiyo iweze kutumia gesi asilia.
Hivi majuzi tu nilizindua ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.  Litakapokamilika nchi yetu itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 3,000 na kuung’oa mzizi wa fitina wa mgao na upungufu wa umeme nchini.  Tumeendelea kuwekeza katika usambazaji wa umeme nchini jambo ambalo limetuwezesha kuwapatia umeme kwa asilimia 18.4 Watanzania kutoka asilimia 10 mwaka 2005.  Kwa kasi hii naamini tutafikia lengo la asilimia 30 ifikapo 2015.
Kwa upande wa maji, jitihada za kuwapatia wananchi maji safi na salama zinaendelea vizuri. Eneo hili lina changamoto kuu mbili.  Kwanza ni ule ukweli kwamba kuna baadhi ya maeneo ya nchi yetu hayana vyanzo vya maji karibu au hayapati mvua za kutosha au yana ukame. Katika maeneo ya aina hii upatikanaji wa maji huwa wa shida sana na hivyo kutulazimisha kujenga miradi ya maji ya bomba kutoka masafa marefu.  Changamoto yetu ya pili ni ule uwezo mdogo wa kifedha kwa miradi mingi inayohitaji pesa nyingi.  Mwaka 2006  tulianzisha Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.  Kufuatia utekelezaji ulio makini wa programu ya sekta ya maji, asilimia 60 ya watu wa vijijini na asilimia 86 ya watu wa mijini wanaopata maji safi na salama.  Ni matumaini yangu kuwa tutafikia lengo letu la asilimia 65 la upatikanaji maji kwa vijijini na asilimia 90 kwa mijini ifikapo 2015. Bahati nzuri tunayo miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini na itapokamilika tutafikia lengo letu au hata kulivuka.
Pongezi kwa Kuchaguliwa
Ndugu Wajumbe;
Katika Mkutano huu, Ndugu Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar na Ndugu Pius Msekwa, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa Tanzania Bara watastaafu.  Ndiyo maana NEC imeamua kuwapendekeza kwenu Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Ndugu Philip Mangula kuchukua nafasi zao.  Napenda kuchukua nafasi hii kwashukuru kw dhati Rais Amani Abeid Karume na Mzee Msekwa kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kunisaidia kuongoza Chama chetu.  Wamekifanyia Chama chetu mambo mengi mazuri ambayo hatuna budi kuwapongeza na kuwashukuru.  Waliendelea kuwa walimu wangu na washauri wangu kwa mambo mengi ya Chama na nchi.  Nawashukuru sana.  Sote tuwatakie afya njema na maisha marefu.  Na tumuombe Mzee Msekwa asichoke kuandika ili hazina yake kubwa ya uzoefu na maarifa iwanufaishe wengi kwa miaka mingi ijayo.
Kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya na Jumuiya pamoja na Wajumbe, nirudie kuwapongeza nyote kwa kuchaguliwa kwenu.  Poleni kwa magumu ya uchaguzi mliyokumbana nayo.  Sasa uchaguzi umeisha, fanyeni kazi ya kujenga Chama.  Tibuni majeraha ya uchaguzi na hasa fanyeni kila muwezalo kuziba nyufa za uchaguzi na migawanyiko miongoni mwa wanachama na viongozi.  Kumbukeni wosia wa Baba wa Taifa “Umoja ni Nguvu”  Kumbukeni kaulimbiu ya Mkutano wetu huu ya Umoja ni Ushindi!  Umoja na Ushindi!  Kajengeni umoja katika maeneo yenu ya uongozi kwa maslahi ya Chama chetu na nchi yetu.
Hitimisho
Ndugu Wana-CCM;
Kwa kuhitimisha naomba nirudie kusema kuwa tumepata mafanikio ya kutia moyo katika ujenzi wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015.  Bado kazi kubwa iko mbele yetu kwa mambo yote hayo mawili.  Tunaitambua na tunayo mipango thabiti ya kutekeleza majukumu yetu.  Nina imani tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kufikia malengo yetu.  Tukiendelea kushirikiana tutafika.  Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!
Baada ya hotuba yangu naomba sasa nitamke kuwa Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM umefunguliwa rasmi.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Kidumu Chama cha Mapinduzi
       Asanteni sana kwa Kunisikiliza                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                
Read more...